SERIKALI YAONDOA USHURU MPYA WA BODABODA

 


SERIKALI imekubali ushauri wa wabunge wa kufuta pendekezo la kuzitoza pikipiki ushuru wa bidhaa wa asilimia tano.

Sambamba na hilo, imefuta mpango wa kuongeza ada ya usajili wa pikipiki kutoka Sh 95,000 hadi Sh 150,000.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar alitangaza uamuzi huo wakati akiwasilisha maelezo ya Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2026 bungeni Dodoma jana.

Balozi Omar alisema serikali imekubaliana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuondoa pendekezo la kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia tano kwenye pikipiki kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye Ibara ya 11(g) ya muswada huo.

Juni 11, mwaka huu, wakati akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2026/2027, waziri alipendekeza kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia tano kwenye pikipiki isipokuwa pikipiki za wagonjwa wa dharura, pikipiki zinazotumia gesi asilia na pikipiki za umeme.

Awali, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ilipinga pendekezo la serikali na kuitaka itafakari upya kwa kusema kwamba pikipiki zimetoa fursa ya ajira kwa vijana wengi.

“Kiwango kinachopendekezwa cha ushuru ni kikubwa kinachoweza kuathiri si tu bei ya pikipiki hizo bali kitaathiri pia ajira za vijana wanaojiajiri kupitia biashara ya kusafirisha abiria,” alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mashimba Ndaki.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando (CCM) alisema, “Hizi tozo zipelekwe sehemu zingine, si mtuletee sisi watu wa tungi (walevi)?... watoleeni bodaboda mtuletee sisi watu wa tungi tutalipa hiyo hela wala haina shida yoyote,” alisema Chipando maarufu kwa jina la Baba Levo.

Mbali na hilo, Balozi Omar alisema Sehemu ya 24 ya Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2026 inapendekeza marekebisho katika Kifungu cha 25 cha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, Sura ya 161 ili kuongeza Sh 20 zinazotozwa katika kila sigara 1,000.

Pia, Sh 20 itatozwa katika kila kilo moja ya sukari inayoagizwa kutoka nje ya nchi kuwa chanzo cha mapato ya Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.

“Lengo la marekebisho haya ni kugharimia huduma ya bima ya afya kwa watu wanaostahili kugharamiwa na mfuko huo,” alisema.

Balozi Omar alisema sehemu ya saba ya muswada huo inapendekeza kufanya marekebisho katika Kifungu cha 34 cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41 ili kuongeza kodi kwenye zawadi ya ushindi katika michezo ya kubahatisha hadi kufikia asilimia 15.

Aliwaeleza wabunge pia kuwa uboreshaji unafanyika kwenye mgawanyo ili kubainisha mgawanyo wa mapato yanayotozwa kwenye zawadi ya ushindi katika michezo ya kubashiri matokeo.

Alisema asilimia saba ya mapato ya kasino za ardhini yanagawanywa kwa asilimia 70 kwenda Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi na asilimia 30 itaelekezwa kwenye Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote.

“Aidha, asilimia 13 ya mapato ya michezo ya kubashiri yanagawanywa kwa asilimia 70 kwenda Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi na asilimia 30 itaelekezwa kwenye Mfuko wa Bima ya Afya kwa Wote,” alisema.

Alisema asilimia 70 ya tozo itawasilishwa moja kwa moja katika Mfuko wa Barabara, asilimia 25 itawasilishwa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali na asilimia tano itawasilishwa katika akaunti maalumu iliyopo BoT kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu saidizi katika maeneo maalumu ya kiuchumi au maeneo ya uzalishaji kwa mauzo ya nje ya nchi

No comments