SERIKALI INAENDELEA NA MABORESHO YA KATIBA
Serikali imesema inaendelea kuonyesha utashi wa kisiasa katika kushughulikia masuala ya maboresho ya Katiba kwa kufuata taratibu na misingi iliyowekwa kisheria ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa shirikishi na wenye manufaa kwa wananchi wote.Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kaskazini kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai na mwelekeo wa Serikali katika masuala ya mageuzi ya kikatiba.
Katambi amesema Serikali imekuwa na dhamira ya kuendeleza maboresho ya Katiba tangu awamu zilizopita, huku hatua mbalimbali zikichukuliwa katika kuendesha mchakato huo.
Amebainisha kuwa wakati wa mchakato wa awali kulijitokeza hoja tofauti kutoka kwa wadau mbalimbali ambazo zilihitaji majadiliano zaidi ili kufikia mwafaka.
Ameongeza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka bayana utaratibu wa kufanya marekebisho, kufuta au kuboresha baadhi ya masharti ya kikatiba kulingana na mahitaji ya jamii na maendeleo ya wakati husika.
Aidha, Katambi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuzingatia sheria, ushirikishwaji wa wananchi na maslahi mapana ya taifa katika hatua zote za maboresho ya Katiba ili kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa utulivu, uwazi na kwa manufaa ya Watanzania wote.

Post a Comment