MRADI WA BBT KUZALISHA AJIRA 6,000


 Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) wa Unenepeshaji wa Mbuzi na Kondoo pamoja na Kilimo cha Malisho, unaotekelezwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, unatarajiwa kuwawezesha wanawake na vijana 6,000 ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wake.

Mradi huo unalenga kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli za ujasiriamali na biashara ya mifugo, sambamba na kukuza ajira na kipato kwa makundi hayo.

Akizungumza mkoani Morogoro katika warsha ya kupitia, kuhakiki na kuwasilisha ripoti ya awali ya Jinsia na Ujumuishaji wa Kijamii katika programu ya BBT, Meneja wa Mradi wa BBT upande wa Jinsia na Ujumuishaji wa Kijamii, Neema Urassa, amesema mradi huo umebuniwa kuwawezesha wanawake na vijana kupitia shughuli za unenepeshaji wa mbuzi na kondoo kibiashara pamoja na kilimo cha malisho ya mifugo.

“Mradi huu unawalenga zaidi wanawake na vijana ambao watapata mafunzo kwa vitendo katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya mifugo, hususan mbuzi, kondoo na kilimo cha malisho. Lengo ni kuwajengea uwezo wa kuingia katika biashara za unenepeshaji wa mifugo kwa ajili ya kujiongezea kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema Urassa.

Ameeleza kuwa baada ya kupata ujuzi huo, vijana watanufaika kwa kujiajiri wenyewe, kuanzisha biashara zao na kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto ya ajira nchini.

Aidha, amesema vijana watakaonufaika na programu hiyo watapata fursa ya kupatiwa mikopo isiyo na dhamana ili kuwawezesha kuendeleza biashara zao baada ya kukamilisha mafunzo, hatua inayotarajiwa kuongeza tija katika sekta ya mifugo na kuimarisha uchumi wa wananchi.

No comments