SAMIA: MANENO BASI, SASA NI UTEKELEZAJI

 


Na Beda Msimbe,TBN, Moscow

Rais Samia Suluhu Hassan amesema wakati umefika kwa Tanzania na Urusi kutekeleza makubaliano na kuacha maneno katika kufanikisha makubaliano yanayokuza biashara na uwekezaji.

Amesema uwekezaji Tanzania unalipa hasa katika mikakati ambayo imelenga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 

Alisema milango ya Tanzania ipo wazi kuona makubaliano ya ujenzi wa viwanda vya dawa, viwatilifu na uwekezaji mwingine unafanywa kazi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Alisema ikiwa sehemu ya kurahisha utekelezaji wa mikataba ya uwekezaji kuanzia Julai 2 mwaka huu Shirika la Ndege (ATCL) litaanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam, Moscow na Zanzibar.

Aidha ni matarajio ya Rais Samia kwamba Shirika la Ndege la Urusi la Azur pia litanza safari hizo. 

Akizungumza na wafanyabiashara juu ya nafasi ya wananchi wa pande zote mbili kunufaika na uhusiano huo, Rais Samia alizungumzia kuhusu uwekezaji wa Urusi nchini Tanzania na kuwaita wafanyabiashara na wawekezaji katika nishati, madini, dawa za binadamu, viwatilifu na kilimo na kusema mabadiliko makubwa yanatakiwa kufanywa ili kupunguza urari wa biashara.

Alisema ujazo wa sasa biashara hauakisi ukweli kuwa kuna nafasi kubwa ya kuwapo kwa maendeleo ya ushirikiano hasa katika n yajna ambazo ni za kimkakati zinazolenga kuihudumia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. 

Naye Waziri wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Urusi, Maxim Reshetnikov amesema amefurahishwa na juhudi za kuifungua Tanzania zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Alisema juhudi hizo zinazaa matunda na kwamba Urusi ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika miradi yake ya kimkakati.

Anasema taifa hilo litaendelea kufungua fursa mbalimbali kwa kuwekeza nchini Tanzania katika kilimo na teknolojia na viwanda 

“Tanzania ni lango la mashariki ya kati tupo tayari kuwapatia teknolojia na utaalamu wetu na tupo tayari kushiriki katika kuanzisha viwanda mbalimbali vya dawa na mbolea” alisisitiza waziri huyo.

Pia akashukuru kwa namna ambavyo wafanyabiashara wa Tanzania walivyofika kwa wingi baada ya mkutano wa Arusha, kushiriki katika ukamilishaji wa mambo mbalimbali.

Aidha mmoja wa wafanyabiashara wa Kitanzania akizungumza baada ya kukamilika kwa kongamano hilo, Dhruv Jog, amesema kualikwa kwa wafanyabiashara katika safari ya Rais na kushiriki kongamano hilo inaonesha ni kwa namna gani sekta binafsi inathaminiwa katika kubadili maisha ya Watanzania.

Alisema kitendo hicho kinasaidia kuifungua jumuiya ya sekta binafsi katika daraja jingine. Alisema kufanikiwa kufungua soko la Urusi kutawezesha watanzania kufanya biashara na nchi takribani 15 zinazofanya ukanda wa Urusi hivyo kuleta kipato zaidi. 

Katika ziara hii ya kihistoria ikifanywa kwa mara ya pili katika historia ya uhusiano wa Tanzania na Urusi, ya kwanza ilikuwa ni miaka ya 1960 iliyofanywa na baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Rais Samia anaendeleza kampeni kubwa ya kuhakikisha Tanzania inanufaika pia kiuchumi na uhusiano mzuri na mataifa mbalimbali.

Akiwa hapa Rais Samia alifanya mazungumzo na Rais Vladmir Putin katika lengo la kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa, kiuchumi na kihistoria baina ya Tanzania na Urusi

Pia Rais Samia ameiweka Tanzania katika ramani ya uwekezaji kwa hotuba yake aliyoitoa katika mkutano mkubwa wa uwekezaji jijini St Petersburg.

No comments