Rais wa Namibia Kurudi Magomeni Alikoishi Miaka ya 1980!

 



Mtaa wa Magomeni Mwembechai jijini Dar es Salaam unatarajiwa kufurika shangwe na nderemo wakati utakapomkaribisha aliyekuwa "jirani" yao wa miaka ya 1980, ambaye sasa anarudi akiwa Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Dkt. Nandi-Ndaitwah anawasili nchini kesho, Juni 19, 2026, kwa ziara ya kitaifa ambapo mbali na kukutana na mwenyeji wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu siku ya Jumamosi, atatenga muda maalum wa kwenda kupaona alipokuwa anaishi Magomeni alipokuwa akipigania uhuru wa nchi yake kupitia chama cha SWAPO.

Huu ni ugeni mzito unaoamsha kumbukumbu za jinsi Dar es Salaam ilivyolea viongozi wakubwa barani Afrika wakati wa harakati za ukombozi. Baada ya Magomeni, Rais huyo pia ataelekea Kongwa, Dodoma kutembelea kambi ya zamani ya wapigania uhuru.

Ratiba ya Ziara ya Kitaifa

  • Juni 19, 2026: Kuwasili nchini kwa Rais Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah.
  • Juni 20, 2026: Mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam, yakifuatiwa na mkutano na waandishi wa habari.
  • Ziara ya Kumbukumbu: Kutembelea Magomeni Mwembechai (Dar es Salaam) na Kambi ya Wapigania Uhuru iliyopo Kongwa, mkoani Dodoma.
  • Juni 22, 2026: Hitimisho la ziara.

"Ziara hii ni dhihirisho la uhusiano wa kindugu na wa kihistoria kati ya Tanzania na Namibia, uliojengwa katika misingi ya harakati za ukombozi wa Afrika, mshikamano na ushirikiano wa maendeleo," ilieleza taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Bakari S. Machumu.

Magomeni kaeni mkao wa kula, 'mtoto wa nyumbani' anarudi akiwa Rais!

 

No comments