RAIS SAMIA APITA NYENDO ZA NYERERE URUSI
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imefufua kumbukumbu za miaka 57 iliyopita wakati Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alipofanya ziara ya kitaifa nchini humo mwaka 1969.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Balozi Kombo amesema viongozi hao wawili wamekuwa na mwelekeo unaofanana katika maeneo matatu makuu ya uchumi, siasa za kimataifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika jukwaa la Dunia.Amesema kama ilivyokuwa kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1969, Rais Samia pia amehutubia katika Jiji la St. Petersburg, ambalo wakati huo lilijulikana kama Leningrad, na kutumia jukwaa hilo kueleza fursa za uwekezaji, biashara na utalii zilizopo Tanzania.
Ameongeza kuwa viongozi hao wote wawili walitumia majukwaa ya kimataifa kueleza msimamo wa Tanzania kuhusu masuala ya dunia na kusisitiza umuhimu wa amani, ushirikiano na maendeleo ya pamoja.
Kwa mujibu wa Balozi Kombo, hatua ya Rais Samia kushiriki Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali ni mwendelezo wa diplomasia ya kimkakati iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, yenye lengo la kuimarisha ushawishi wa Tanzania na kufungua fursa zaidi za maendeleo.

Post a Comment