ZINDUKA MTANZANIA: VYOMBO VYA HABARI VYA NJE VINA AJENDA YA KUCHAFUA SIFA YETU



Mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji, ametoa wito mzito kwa Watanzania kuwa waangalifu na vyombo vya habari vya kimataifa, akivituhumu kuwa na ajenda ya makusudi ya kuchafua taswira ya Tanzania badala ya kuripoti maendeleo makubwa yaliyofikiwa. 

Katika msimamo wake usio na shaka, Dewji ameeleza kuwa vyombo kama BBC na vingine vinaendesha shughuli zao kwa gharama kubwa sana, wakitangaza habari katika lugha nyingi bila ufafanuzi wa wazi wa namna wanavyofidia gharama hizo, jambo ambalo linaibua maswali kuhusu nia yao halisi. 

Amesema kuwa vyombo hivyo havioni wala kutangaza mafanikio makubwa ya Tanzania katika sekta za miundombinu kama SGR, upatikanaji wa umeme, na huduma nyingine za kijamii, bali vimejikita katika kupotosha ukweli kwa lengo la kuleta fitina na kugombanisha wananchi.

Dewji ameweka wazi kuwa Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa mbinu hizi za vyombo vya nje ni mwendelezo wa jitihada za kibeberu zinazotaka kuendeleza ukoloni mamboleo kwa kutaka Watanzania waamini na kufuata kila wanachokisema wao. 

Amesistiza kuwa ni hatari kwa wananchi kuamini kila taarifa inayotoka nje bila kuzifanyia tathmini, akionya kuwa taifa lina kila sababu ya kulinda mshikamano wake dhidi ya maadui wanaotumia uongo na uzushi kama silaha ya kudhoofisha nchi. 

Kama kielelezo cha upotoshaji huo, ametolea mfano wa jinsi vyombo hivyo vilivyowahi kutoa taarifa za uongo kuhusu uwepo wa makaburi ya watu wengi nchini, jambo ambalo ni la uzushi mtupu lililolenga kuichafua nchi kimataifa bila ushahidi wowote.

Kwa kuzingatia athari hizo, mfanyabiashara huyo ameshauri Serikali kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya vyombo hivyo vinavyovuka mipaka ya taaluma na kuingia katika uchochezi wa moja kwa moja. 

Amehoji uhalali wa vyombo hivyo vinavyoripoti mambo ya Tanzania wakiwa wamejificha nje ya mipaka, akisisitiza kuwa ni vyema zaidi Watanzania wajikite kusikiliza na kuamini taarifa zinazotoka ndani ya nchi, ambapo kuna mifumo ya kisheria inayoweza kuwawajibisha wale wote wanaopotosha ukweli. 

Aidha amewataka Watanzania kuwa na uzalendo wa dhati kwa kuikataa ajenda ya kugombanishwa na wageni wanaotaka kuona nchi ikiyumba, huku akisisitiza kuwa Tanzania ina mambo mengi mazuri ya kujivunia ambayo hayapaswi kufunikwa na uongo wa vyombo vya habari vya kimataifa.

No comments