KIHONGOSI ATAKA AMANI KULINDWA




Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amewataka wananchi wa Hanang' mkoani Manyara kutokubali kushawishiwa kuvunja amani, badala yake wajikite katika shughuli za maendeleo na kujiongezea kipato.


Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Hanang', Kihongosi amesema muda wa kufanya vurugu haupo na kwamba kila mwananchi anapaswa kuelekeza nguvu zake katika kutafuta uchumi na kuboresha maisha yake.

Pia Kihongosi alisema maendeleo ya kweli hupatikana kupitia kazi, uzalishaji na shughuli za kiuchumi, huku akiwahimiza wakulima, wafanyabiashara na waendesha bodaboda kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuboresha maisha yao.
Amehimiza wakulima, wafanyabiashara na waendesha bodaboda kufanya kazi kwa bidii ili kuongeza kipato na kuinua ustawi wa familia zao, badala ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano ili kuendelea kujenga taifa lenye maendeleo na ustawi kwa wananchi wote.

Pia Kihongosi alifikisha salamu za Rais na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan kwa wananchi hao akisema Rais anawashukuru wananchi wa Manyara kwa kuendelea kumuunga mkono na kwamba anatarajia kufanya ziara katika mikoa ya Kaskazini siku zijazo.

Katika mkutano huo, wananchi kupitia Mwenyekiti wa Shina Namba Moja, Maria Paulo, waliwasilisha ombi la kupandishwa hadhi kwa zahanati ya Masakta kuwa kituo cha afya kutokana na ongezeko la idadi ya watu na mahitaji makubwa ya huduma za afya, ikiwemo huduma za mama na mtoto, upasuaji pamoja na makazi ya watumishi wa afya.

Akijibu ombi hilo, Kihongosi alisema CCM itasimamia suala hilo endapo vigezo vinavyotakiwa vitakuwa vimetimizwa, huku akiwataka viongozi wa Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Hanang’ pamoja na Mbunge wa eneo hilo kushirikiana kuhakikisha changamoto hiyo inapata ufumbuzi.

Ziara hiyo imeendelea kuonyesha uimara wa CCM katika Wilaya ya Hanang’, huku wananchi wakieleza kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika kuleta maendeleo ya eneo lao.

No comments