MAMILIONI YA WHICKERS YATUA TANZANIA KUKAMILISHA FILAMU YA CHIDREN OF HONEY



Na Rahel Pallangyo

Filamu ya Kitanzania ya Children of Honey imejipatia ruzuku nono ya pauni 120,000 za Uingereza, ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 400 za Kitanzania, baada ya kushinda tunzo ya 2026 ya Whickers Film & TV Funding Award ya Uingereza.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi 600 duniani kote iliyoomba kufadhiliwa ukamilishaji wake.

Waongozaji wenza, Jigar Ganatra na Emanuel Musa Marco,walipigania vilivyo mradi wao wakati walipoingia katika hatua za tano bora kati ya maingizo 600.

Kazi ya kupigania mradi huo waliifanya kwenye jukwaa kubwa la tamasha la Sheffield DocFest—ambalo ni moja ya masoko yenye ushawishi mkubwa zaidi wa filamu za dokumentari duniani.

Baada ya mchujano huo wa awali ulioweka kando mamia ya washiriki, ni miradi mitano tu ya kipekee iliyoalikwa nchini Uingereza ukiwamo wa Children of Honey na kuchuana katika jukwaa hilo mbele ya jopo la majaji waliobobea, akiwemo mwandaaji wa filamu kutoka Kenya Sam Soko na mkurugenzi wa ubunifu wa Sheffield DocFest, Raul Niño Zambrano.

Katika fainali hiyo ya kukata na shoka, Tanzania ilichuana bega kwa bega na filamu kutoka mataifa makubwa zikiwemo Welcome to Our Bathhouse kutoka Japan, Ashes kutoka Syria, Mexico is Ours kutoka Scotland, na All Fixed Up kutoka China, ambapo kila mshiriki alipewa dakika saba tu za kusimama jukwaani kuwasilisha wazo lake na vionjo vya video, kisha kukabiliwa na maswali magumu ya papo kwa papo kutoka kwa majaji ili kutetea sanaa yake.

Filamu ya Children of Honey, iliyoundwa kwa ushirikiano wa karibu na jamii ya wawindaji na waokotaji matunda ya Wahadzabe wa kaskazini mwa Tanzania, imeweka rekodi ya kuwa filamu ya kwanza ya ukweli ya urefu wa kati kuongozwa kwa ushirikiano na mwandaaji anayetokea ndani ya jamii hiyo yenyewe.

Hadithi hii inafuatilia kwa ukaribu maisha ya vijana watatu wa Kihadza wanapopita katika kipindi cha mpito kuelekea utu uzima, huku wakikabiliwa na mabadiliko makubwa ya kijamii na kiutamaduni yanayotishia mazingira yao ya asili.

Kupitia mfumo huu bunifu wa ushirikishwaji, Wahadzabe wenyewe si tu wahusika wa filamu bali ni wasimulizi wakuu wa hadithi yao, wakitumia vifaa vya kurekodi na picha walizopiga wenyewe ili kuonesha taswira halisi ya maisha, mila, na mustakabali wao kwa ulimwengu.

Kupatikana kwa ruzuku hii sasa kunafungua milango ya kuendeleza uzalishaji wa Children of Honey, huku ukiongeza nguvu katika kampeni ya uhifadhi wa lugha na utamaduni wao, wakati filamu ya Kijapani ya Welcome to Our Bathhouse ikishika nafasi ya pili na kuondoka na pauni elfu ishirini na tano.

No comments