Machozi, Shangwe na Kumbukumbu Rais wa Namibia aliporejea Magomeni kukutana na majirani wake wa zamani




Machozi ya furaha na hisia nzito zilitawala anga la Magomeni jijini Dar es Salaam, pale Rais wa Namibia, Dk. Netumbo Nandi-Ndaitwah, aliposhuka kwenye gari lake na kukutana uso kwa uso na wapendwa wake wa zamani hasa nMama Salehe pamoja na mtoto wa marehemu Mama Salama. 

Ukiangalia nyuso za hao wakati wanakutana unapata picha ya kusisimua iliyorejesha nyuma gurudumu la muda hadi miaka ya dhiki na mapambano.

Waliposalimiana unaona kabisa haikuwa tu salamu kati ya Rais na raia, bali ilikuwa ni muunganiko wa mioyo iliyoshibana kwa upendo wakati wa ujirani kipindi cha harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. 

Akizungumza na wakazi hao, Rais huyo alitoa shukurani zake kwa serikali na wananchi wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika harakati za ukombozi wa Namibia, akisisitiza kuwa historia hiyo imejenga uhusiano imara na wa kudumu kati ya mataifa hayo mawili.

 “Magomeni ni sehemu ya maisha yangu na historia ya taifa langu. Tanzania ilitupa hifadhi, upendo na nafasi ya kupigania uhuru wetu. Huu ni ushahidi wa urafiki wa kweli na mshikamano wa Afrika,” alisisitiza. 

“Ziara yangu hapa leo ni ushahidi usiofutika wa urafiki wa dhati na mshikamano wa kweli wa Kiafrika,” alisisitiza Rais Nandi-Ndaitwah.









Majirani hawa wa zamani walimwangalia mwanamke huyu aliyekuwa kijana mwanaharakati wa Chama cha SWAPO, sasa akiwa kiongozi mkuu wa nchi, lakini bado akiwa na tabasamu lilelile la unyenyekevu lililomstiri miaka mingi iliyopita kwenye korido za nyumba hiyo ya uswahilini.

Katikati ya shangwe na vigelegele vya wakazi waliomiminika kushuhudia tukio hilo la kipekee, kwa hakika Rais Nandi-Ndaitwah alishindwa kuficha mguso wa moyo wake alipokiri kuwa Magomeni ni sehemu isiyofutika ya maisha yake na msingi imara wa historia ya taifa la Namibia. Alikumbuka kwa shukrani jinsi Tanzania isivyowapa hifadhi pekee, bali iliwakumbatia kwa upendo wa dhati na kuwapa jukwaa salama la kupigania uhuru wao dhidi ya utawala wa kibaguzi. 

Baada ya dakika kadhaa za kubadilishana maneno ya faraja na majirani hao waliomshika mikono kwa  fahari, kiongozi huyo alipiga hatua na kuingia ndani ya vyumba vya nyumba hiyo aliyowahi kuishi, akivuta picha ya mikakati, ndoto na changamoto za miaka ile ya mapambano, huku wenyeji wake wakibubujikwa na furaha kuona kuwa mtoto wao wa zamani amerudi nyumbani akiwa Rais, lakini hajasahau asili yake wala watu waliomfariji wakati wa dhiki.

Majirani hao walieleza kufurahi kwao kuona mtoto wao wa zamani amerudi akiwa Rais wa nchi, lakini bado hajasahau asili na watu waliomstiri.


No comments