Kutoka Magomeni hadi Kongwa: Rais wa Namibia Azidisha Hisia za Kihistoria na Urafiki wa Damu Nchini Tanzania

 


Safari ya kihistoria na iliyojaa mguso wa kipekee wa kiitikadi na kibinadamu ya Rais wa Namibia, Dk. Netumbo Nandi-Ndaitwah nchini Tanzania imeendelea kuamsha kumbukumbu nzito za harakati za ukombozi, safari hii ikihamia makao makuu ya nchi mkoani Dodoma baada ya kuacha alama ya upendo na machozi ya furaha jijini Dar es Salaam. 

Kiongozi huyo, ambaye leo pale Magomeni aligusa nyoyo za wengi kwa kutembelea nyumba ya uswahilini aliyowahi kuishi  na kusalimiana  kwa hisia na majirani zake wa zamani, aliwasili kwenye Kiwanja cha Ndege cha Dodoma majira ya mchana na kuendelea na ziara yake ya kitaifa, ambapo alipokelewa kwa heshima zote na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi. 

Ziara hii ya kikazi inazidi kudhihirisha undugu usiofutika kati ya mataifa haya mawili, uliomwagikiwa damu na jasho wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Namibia kupitia Chama cha SWAPO chini ya mwavuli na hifadhi ya ukarimu ya Tanzania.



Kama sehemu ya kuacha kumbukumbu ya kudumu ya kidiplomasia katika mji mkuu huo mpya, Rais Nandi-Ndaitwah alipata fursa ya kupanda mti katika Mji wa Serikali Mtumba, eneo maalum lililotengwa kwa ajili ya Kiwanja cha Ubalozi wa Namibia, kama ishara ya kukuza na kushamiri kwa uhusiano wa mataifa haya mawili ya Afrika.

Baadaye, kiongozi huyo alielekea wilayani Kongwa katika Kambi maarufu ya Wapigania Uhuru, mahali ambapo historia ya ukombozi ilipikwa na kulindwa, na huko alikabiliwa na wakati mwingine mzito wa kihisia pale alipotembelea makaburi ya wanaharakati wenzake wa SWAPO waliofia vitani.







Akiwa ameambatana na viongozi waandamizi wa Tanzania wakiwemo Profesa Kabudi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, Rais Netumbo alipatiwa maelezo ya kina kuhusu kambi hiyo kabla ya kusimama kwa unyenyekevu na kutoa heshima zake za mwisho, kisha akaweka shada la maua kwenye moja ya makaburi hayo ya mashujaa wa ukombozi, akithibitisha kwa vitendo kuwa Tanzania itabaki kuwa chemchemi na nguzo kuu ya uhuru wa Namibia.

No comments