CHUO CHA DHOW COUNTRIES MUSIC ACADEMY CHA ZANZIBAR CHASHINDA TUZO YA UNESCO-SHARJAH YA UTAMADUNI



Paris, Ufaransa

Chuo cha Dhow Countries Music Academy (DCMA) cha Zanzibar kimeandika historia baada ya kutangazwa mshindi wa Tuzo ya 21 ya UNESCO-Sharjah Prize for Arab Culture, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya UNESCO jijini Paris, Ufaransa. Chuo hicho kimetunukiwa tuzo hiyo kutokana na mchango wake mkubwa katika kuhifadhi, kufundisha na kuendeleza urithi wa muziki wa taarab na tamaduni za ukanda wa Bahari ya Hindi na Kiarabu.  

Mwakilishi wa chuo hicho, Bi. Haldah Am Al-Kanaan, alikuwepo Paris kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya taasisi. DCMA ni chuo pekee cha muziki Zanzibar kinachojikita katika kufundisha ala za asili na mitindo ya muziki wa jadi ikiwemo taarab, kidumbak na ngoma, huku kikileta pamoja wanafunzi kutoka mataifa mbalimbali na rika tofauti.  

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, Profesa Khaled El-Enany, alikipongeza chuo hicho kwa ubunifu wake katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa muziki wa Kiarabu na Kiswahili. Alisema majaji kutoka mabara mbalimbali walivutiwa na namna DCMA ilivyoweza kutumia muziki kama daraja la kuunganisha tamaduni tofauti, pamoja na mazingira yake ya kujifunzia yanayowakutanisha wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali duniani.  




Kwa upande wake, uongozi wa DCMA ulieleza kuwa tuzo hiyo ni heshima kubwa kwa Zanzibar na Tanzania, na kwamba itakuwa chachu ya kuongeza juhudi katika kulinda na kuendeleza urithi wa taarab na muziki wa jadi kwa vizazi vijavyo.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu katika UNESCO, Balozi Saidi Othman Yakubu, ambaye alishuhudia tukio hilo la kihistoria na kuwapongeza washindi kwa kuitangaza vyema Tanzania kupitia sanaa na utamaduni katika jukwaa la kimataifa.

Tuzo ya UNESCO-Sharjah Prize for Arab Culture, iliyoanzishwa mwaka 1998 kwa ushirikiano kati ya UNESCO na Serikali ya Sharjah, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), hutolewa kila mwaka kwa watu binafsi au taasisi zilizotoa mchango wa kipekee katika kuendeleza na kutangaza utamaduni wa Kiarabu na kuimarisha mazungumzo ya tamaduni duniani. Katika toleo la mwaka huu, DCMA ilitangazwa mshindi pamoja na mwanamuziki na mjasiriamali wa utamaduni kutoka Morocco, Brahim El Mazned.

No comments