BAJETI 2026/2027: Serikali Kutumia 'Akili Unde' (AI) na Big Data Kudhibiti Uvuja wa Kodi



Serikali imetangaza kuingia kwenye zama mpya ya matumizi ya teknolojia ya juu kwa kuanza kutumia mifumo ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) na Uchambuzi wa Data Kubwa (Big Data) ili kurahisisha utozaji kodi, kudhibiti uvuja wa mapato, na kurasimisha sekta zisizo rasmi nchini. 

Hatua hii inakwenda sambamba na dhima kuu ya bajeti ya mwaka 2026/27 inayolenga kujenga uchumi himilivu kupitia mageuzi ya kidijitali.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ameliambia Bunge kuwa Serikali inapitia mifumo yake yote ya kielektroniki ili kuifanya isomeane. 

Katika mkakati huo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeagizwa kutengeneza programu tumizi (application) maalum ya simu za mkononi na vishikwambi itakayotolewa bure kwa wafanyabiashara ili itumike kutoa risiti za kielektroniki bila ulazima wa kununua mashine za EFD.

Mageuzi haya pia yanahusisha Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, ambayo itaongeza moduli maalum katika mfumo maarufu wa TAUSI. 

Moduli hiyo itawawezesha watendaji wa mitaa na vijiji kusajili wafanyabiashara wote katika maeneo yao kwa urahisi, wakiwemo wale ambao hawajafikia viwango vya kuwa na leseni rasmi za biashara.

Ili kuondoa kero na urasimu kwa sekta binafsi, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanzisha Mfumo wa Pamoja wa Malipo (Single Window Payment System). 

Mfumo huu utajumuisha ada, tozo, na adhabu zote zinazotolewa na taasisi mbalimbali za udhibiti nchini kama vile EWURA, LATRA, TCRA, na TCAA, na hivyo kumfanya mfanyabiashara kufanya malipo yake yote katika dirisha moja.

No comments