BAJETI 2026/2027 : ULINZI WA VIWANDA VYA NDANI NA NISHATI SAFI VYATAWALA
Katika jitihada za kulinda ajira za ndani, kuzuia uvuja wa fedha za kigeni, na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, Serikali imetangaza hatua kali na madhubuti za kikodi kupitia Bajeti Kuu ya mwaka 2026/27. Hatua hizo zinalenga kukuza tasnia ya uzalishaji wa bidhaa nchini ili nchi iache kutegemea uagizaji kutoka nje.
Akiwasilisha hotuba hiyo, Waziri wa
Fedha amependekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Uwekezaji na Maeneo
Maalum ya Kiuchumi ya Mwaka 2024, kwa kuingiza vichwa vya trela (road tractors
for semi-trailers) kwenye orodha ya bidhaa zisizostahili kupata msamaha wa kodi
(negative list). Hatua hii inalenga kulinda viwanda vya ndani vinavyounda trela
hizo na kulinda ajira za mamia ya vijana wa Kitanzania.
Upande wa nishati safi na utunzaji wa mazingira, Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye uingizaji na usambazaji wa mita janja za gesi ya kupikia (LPG smart meters). Pia, msamaha kama huo wa VAT umetolewa kwa vifaa vitakavyotumika katika ujenzi wa vituo vya kuchaji magari yanayotumia umeme (electric vehicles charging stations).
Hatua hizi zinaenda sambamba na agizo la serikali kwa taasisi zote
za umma kuanza kununua magari yanayotumia teknolojia ya umeme na gesi asilia.
Katika kulinda walaji na wakulima wa ndani, Serikali imetangaza kuendelea kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 35 au dola za Marekani 300 kwa tani moja ya mafuta safi ya kula yanayotoka nje (refined edible oil).
Hatua hii inaenda sambamba na kutoa unafuu
wa kodi kwa wazalishaji wa ndani wanaotumia mbegu za alizeti, pamba, na
michikichi zilizolimwa nchini ili kushusha bei ya mafuta ya kula sokoni.
Post a Comment