TASNIA YA UREMBO KUCHANGIA KUKUZA UCHUMI WA UBUNIFU NA AJIRA NCHINI




Mkurugenzi wa Miss Universe Tanzania, Millen Magese, amebainisha kuwa sekta ya urembo nchini ina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira kwa vijana na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa ubunifu endapo itapewa kipaumbele na nafasi stahiki. 

Millen ameeleza kufurahishwa kwake na namna tasnia hiyo inavyoanza kutambuliwa kama sekta muhimu kiuchumi inayoweza kuitangaza Tanzania katika majukwaa ya kimataifa, akisisitiza kuwa urembo si suala la mwonekano pekee bali ni nyenzo yenye nguvu katika ushawishi, utamaduni, na diplomasia.

Akizungumza kufuatia uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 mjini Dodoma, Millen amepongeza hatua za serikali kwa kuonesha nia ya kushirikiana na wadau wa sekta hiyo. 

Amesema kuwa ushirikiano huo ni chachu itakayochochea maendeleo ya tasnia ya urembo na sanaa, huku akibainisha kuwa Miss Universe Tanzania imeanza kurejesha hadhi yake kimataifa na inajipanga kufanya vizuri zaidi katika miaka ijayo ili kuimarisha utambulisho wa taifa duniani.

No comments