DC MPOGOLO AWATAKA WAZAZI ILALA KUACHA TABIA YA KUWATUMA BODABODA VIKAO VYA SHULE
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka wazazi na walezi mkoani Dar es Salaam kuacha tabia ya kukwepa vikao vya shule na badala yake washiriki kikamilifu katika kufuatilia malezi na maendeleo ya taaluma ya watoto wao.
Akizungumza katika Shule ya Sekondari Zawadi iliyopo Tabata, Mpogolo amebainisha kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanategemea ushirikiano wa pande tatu ambao ni Serikali inayoboresha miundombinu na walimu, wazazi wanaosimamia malezi, pamoja na wanafunzi wenyewe wanaopaswa kuwa na nidhamu na bidii katika masomo.
Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kusikitishwa na mwitikio mdogo wa wazazi katika shule za Serikali, ambapo baadhi yao wamekuwa na tabia ya kuwatuma ndugu, wafanyakazi wa nyumbani, au hata madereva wa bodaboda kuwawakilisha kwenye vikao vya maendeleo ya wanafunzi.
Alisema serikali ina jukumu la kuboresha miundombinu na kuhakikisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia kupitia walimu,huku wazazi na jamii wakipaswa kusimamia malezi na kufuatilia mwenendo wa watoto wao.
Aidha, alisema wanafunzi wanapaswa kuwa na nidhamu, kuzingatia maadili mema na kuongeza bidii katika masomo yao.
“Tunapozungumzia mafanikio ya mtoto lazima tuzungumzie maeneo matatu makubwa. Serikali ina wajibu wake kupitia walimu, wazazi wana wajibu wao, na wanafunzi nao wanapaswa kuwa na nidhamu na bidii,” alisema Mpogolo.
“Hivyo ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu na wanafunzi ni muhimu sana katika kuhakikisha mtoto anafanya vizuri kitaaluma na kimaadili,”aliongeza.
Ameonya kuwa kukosekana kwa ushirikiano kunaathiri mwenendo wa kitaaluma na kimaadili wa mtoto kwa kuwa ushirikiano wa moja kwa moja kati ya mzazi na mwalimu unakosekana, tofauti na ilivyo katika shule binafsi ambako wazazi hujitokeza kwa wingi.
Katika kuhakikisha hali hiyo inabadilika, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imedhamiria kuimarisha ushiriki wa viongozi katika vikao vya wazazi ili kuongeza hamasa na umuhimu wa ufuatiliaji wa elimu.
Alisema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imedhamiria kuimarisha ushiriki wa viongozi katika vikao vya wazazi ili kuongeza hamasa ya kufuatilia maendeleo ya wanafunzi.

Post a Comment