TANZANIA YA TATU DUNIANI SOKO LA UTALII LILILOFANYA VYEMA KATIKA MATUMIZI YA FEDHA

 


Sekta ya maliasili na utalii nchini Tanzania imeweka rekodi mpya ya kihistoria baada ya kutangazwa kuwa nchi ya tatu duniani kwa soko la utalii lililofanya vizuri zaidi katika matumizi ya fedha (best performing market by spending). Mafanikio hayo makubwa yamebainishwa leo bungeni jijini Dodoma wakati wa uwasilishaji wa hotuba ya Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na Waziri wa sekta hiyo, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji.

Hatua hii inafuatia ripoti iliyotolewa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) ya Januari 2026, ambayo imeonyesha kuwa Tanzania imekuwa kivutio kikubwa kwa watalii wenye uwezo mkubwa wa kifedha (high-spenders). Katika bara zima la Afrika, ni mataifa mawili tu yaliyoingia kwenye orodha ya 20 bora duniani, ambapo Tanzania inaongoza ikifuatiwa na kigogo wa zamani wa utalii, Morocco, ulioshika nafasi ya tisa, huku mataifa yote jirani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yakiwa hayakuambulia nafasi hata moja kwenye orodha hiyo.


Maono ya "The Royal Tour" na Ukuaji wa Mapato

Katika mjadala wa bajeti hiyo, Wabunge waliochangia wametoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake ya kimkakati ya kuandaa na kushiriki yeye mwenyewe katika filamu maarufu duniani ya Tanzania: The Royal Tour. Maamuzi hayo ya Rais yanatajwa kuwa chachu kuu iliyoleta mapinduzi haya ya kiuchumi na kuifanya dunia nzima ielekeze macho yake nchini Tanzania.

Kutokana na juhudi hizo, mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kwa asilimia 12.82, ambapo yamepanda kutoka Dola za Marekani bilioni 3.9 mwaka 2024 hadi kufikia Dola bilioni 4.4 mwaka 2025. Ongezeko hili linamaanisha kuwa watalii wanaoingia nchini kwa sasa hawaji tu kupiga picha, bali wanatumia fedha nyingi kwenye huduma mbalimbali, jambo linalochochea ukuaji wa uchumi wa ndani.


Rekodi ya Idadi ya Watalii na Diplomasia

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa Tanzania imeshuhudia ongezeko la kihistoria la wageni, ambapo jumla ya watalii walioingia nchini mwaka 2025 ilifikia 5,935,561 ikilinganishwa na milioni 5.3 ya mwaka 2024. Watalii hawa kwa pamoja wameacha nchini jumla ya Shilingi trilioni 11.4. Sambamba na wageni wa nje, utalii wa ndani nao umekua kwa asilimia 13.1 baada ya Watanzania milioni 3.6 kutembelea vivutio vyao vya ndani, ishara ya kuongezeka kwa uelewa wa kulinda urithi wa taifa.

Ukuaji huu wa asilimia 51 ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya mlipuko wa UVIKO (2019), unaifanya Tanzania kuwa nchi ya 11 duniani na ya 6 katika kanda ya Afrika na Mashariki ya Kati kwa kasi ya ukuaji wa wageni wa kimataifa. Ndani ya kipindi hiki, Tanzania imeshinda tuzo ya nchi bora ya Utalii wa Safari Duniani kupitia World Travel Awards kwa mara ya tatu mfululizo (2023–2025), huku Hifadhi ya Serengeti ikizidi kung'ara kimataifa.


Mikakati Mpya, Miundombinu na Matukio Makubwa

Ili kuendeleza kishindo hiki, Serikali imekamilisha ujenzi wa viwanja vya ndege katika Hifadhi za Taifa za Nyerere na Ruaha, huku uboreshaji wa miundombinu katika Hifadhi ya Mikumi ukitazamiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2026. Lengo kuu la serikali ni kuifanya sekta ya utalii ichangie asilimia 20 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030, kupitia mbinu mpya ya Utalii wa Mikutano na Matukio (MICE).

Kuelekea lengo hilo, Tanzania inajipanga kuwa mwenyeji wa matukio makubwa ya kimataifa, ikiwemo mikutano ya IPU mwezi Oktoba 2026, tuzo za World Travel Awards mwezi Desemba 2026, na mashindano ya ulimbwende ya Miss World mwaka 2027. Aidha, fursa ya kipekee inatarajiwa kupitia mashindano ya soka ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji mwenza, na Wabunge wameiomba Wizara kusimamia kikamilifu utalii wa michezo ili kuvutia mashabiki wengi zaidi.


Bajeti na Ushauri wa Kulinda Taswira ya Nchi

Kwa ajili ya mwaka wa fedha wa 2026/2027, Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kukusanya maduhuli ya jumla ya Shilingi 1,486,502,065,176.69 (Trilioni 1.48). Katika makusanyo hayo, Waziri Dkt. Ashatu Kijaji ameomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 334,345,870,000.00 (sawa na asilimia 22.5) kwa ajili ya uendeshaji, utangazaji wa utalii, na uwekezaji wa kimkakati, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Pamoja na mafanikio hayo, wataalamu wa tasnia wamesisitiza haja ya kuwa na mikakati endelevu. Profesa Jafari Kideghesho, mtaalamu wa Baiolojia ya Uhifadhi na aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Wanyamapori, ameshauri kuwa taifa linapaswa kuweka nguvu kubwa kulinda taswira yake (reputation management). Alionya kuwa mitazamo hasi au upotoshaji unaweza kubomoa mafanikio ya miaka mingi kwa haraka, hivyo serikali lazima iwe wepesi kujibu upotoshaji huo na kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari vya kimataifa kusambaza simulizi nzuri kutoka kwa watalii walioridhika.


Extract kutoka kwa Derek K. Murusuri, Dispatch, Dodoma 

No comments