Kilimo na Ufugaji: Fursa Muhimu kwa Vijana katika Uchumi wa Tanzania
Changamoto kubwa iliyopo si ukosefu wa fursa, bali ni namna ya kuzitumia kwa maarifa, teknolojia na mipango ya kibiashara ambapo kijana anayechanganya elimu, ubunifu na nidhamu ya kazi anaweza kutumia ardhi, mifugo na masoko yaliyopo kujenga maisha bora na kuchangia maendeleo ya taifa.
Ukweli wa takwimu unaonyesha kuwa vijana wanaoamua kuwekeza katika kilimo na ufugaji wanaingia katika sekta yenye nafasi kubwa ya ukuaji kwani kilimo kinaendelea kuwa mhimili muhimu wa uchumi wa Tanzania, kikichangia takribani asilimia 26.3 ya Pato la Taifa mwaka 2024 na kutoa ajira kwa sehemu kubwa ya nguvu kazi nchini.
Kwa upande wa ufugaji, Tanzania ina rasilimali kubwa inayotoa fursa kwa vijana kujenga biashara mbalimbali kuanzia uzalishaji wa nyama, maziwa, mayai, ngozi, usindikaji wa bidhaa za mifugo hadi biashara ya pembejeo kwa kuwa nchi ina zaidi ya ng'ombe milioni 36.6, idadi inayoiweka miongoni mwa nchi zenye mifugo mingi barani Afrika huku sekta hiyo ikitoa fursa za kipato kwa takribani asilimia 33 ya wananchi, sawa na kaya milioni 4.6 zinazohusika katika mnyororo wa thamani wa mifugo. Takwimu hizi zinaonyesha kuwa fursa hazipo kwenye kufuga au kulima pekee, bali zipo katika hatua zote za mnyororo wa thamani ambapo kijana anaweza kuingia kwenye uzalishaji wa mbegu bora, huduma za ugani, teknolojia za kilimo, usindikaji wa mazao, uhifadhi, usafirishaji, masoko ya kidijitali na uuzaji wa bidhaa ndani na nje ya nchi.
Sekta ya mifugo bado ina nafasi kubwa ya kuongezeka kwa tija na licha ya kuwa na idadi kubwa ya mifugo, mchango wake katika uchumi unaweza kuongezwa zaidi kupitia uwekezaji katika ufugaji wa kisasa, uzalishaji wa maziwa, uboreshaji wa mifugo, viwanda vya nyama na bidhaa zinazotokana na ngozi. Kwa vijana, takwimu hizi zinapaswa kuwa ujumbe wa kubadili mtazamo kwa sababu kilimo na ufugaji wa kisasa si shughuli za maisha ya kujikimu pekee, bali ni sekta zenye uwezo wa kuzalisha mamilionea wapya, makampuni ya kilimo, ajira na suluhisho la changamoto za chakula nchini.

Post a Comment