Dkt. Kikwete awasili Botswana kumwakilisha Rais Samia mazishi ya Hayati Festus Mogae

 


Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewasili jijini Gaborone leo Mei 15, 2026, kumwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu wa Botswana, Hayati Festus Gontebanye Mogae. 

Kiongozi huyo wa zamani wa Botswana alifariki dunia Mei 8, 2026, akiwa na umri wa miaka 86, na anatarajiwa kuzikwa kesho Mei 16, jijini humo.

Mara baada ya kuwasili nchini humo, Dkt. Kikwete alifika katika Ukumbi wa Bunge la Botswana ambapo alisaini kitabu cha rambirambi na kuenzi mchango mkubwa wa Hayati Mogae kwa taifa lake na bara la Afrika. 

Wakati wa uandishi wa kitabu hicho, Rais Mstaafu alikuwa ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Botswana, James Bwana.

Katika hatua nyingine ya mapokezi hayo, Dkt. Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Botswana, Dithapelo Keorapetse, pamoja na Katibu wa Bunge hilo, Dkt. Gabriel Goitsemodimo Gosiame Malebang. 

Viongozi wengine waliohudhuria mapokezi hayo ni Balozi James Bwana na Balozi Mstaafu Dkt. Athalia Molokomme, aliyemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana.


No comments