Sir Alex Ferguson akimbizwa hospitali kwa matibabu ya dharura
Kocha wa zamani wa klabu ya Manchester United, Sir Alex Ferguson, anaripotiwa kuendelea vizuri na kurejea katika hali ya kawaida baada ya kukimbizwa hospitalini kwa matibabu ya dharura kabla ya mchezo wa Ligi Kuu ya Uingereza kati ya Man United dhidi ya Liverpool.
Gwiji huyo mwenye umri wa miaka 84 alitafuta huduma ya matibabu ya tahadhari akiwa uwanjani Old Trafford muda mfupi kabla ya mchezo huo kuanza, hali iliyozua hofu miongoni mwa wadau wa soka.
Taarifa kutoka kwa vyanzo vya karibu zimebainisha kuwa kocha huyo yuko salama na anaendelea kupata nafuu kufuatia hatua hizo za kitabibu zilizochukuliwa mapema.
Kabla ya kuanza kuhisi mabadiliko ya afya yake, Ferguson alionekana kwenye mitandao ya kijamii akiwasalimia wageni mbalimbali uwanjani hapo kama ilivyo desturi yake ya kuhudhuria michezo ya klabu hiyo.
Inafahamika kuwa mara baada ya kujihisi vibaya, alifanyiwa uchunguzi wa awali katika eneo la vyumba vya kubadilishia nguo (tunnel) kabla ya kusafirishwa kwa gari la wagonjwa kuelekea hospitalini kwa uangalizi zaidi. Tukio hilo lilitokea takriban saa moja kabla ya mpira kuanza, jambo ambalo lilileta simanzi kwa benchi la ufundi na wachezaji waliokuwa wakijiandaa kwa mtanange huo muhimu.
Kocha mkuu wa sasa wa Manchester United, Michael Carrick, ambaye aliwahi kucheza chini ya Ferguson, alikiri kuguswa sana na taarifa hizo kabla ya kuanza kwa mchezo huo uliomalizika kwa United kushinda mabao matatu kwa mawili.
Carrick alieleza kuwa ingawa hakuwa na taarifa za hivi punde wakati mchezo ukiisha, alikuwa na matumaini makubwa kuwa ushindi huo dhidi ya wapinzani wao wakubwa utakuwa kichocheo cha haraka katika mchakato wa kuimarika kwa afya ya kocha huyo mahiri. Alimalizia kwa kutoa heri na dua kwa niaba ya klabu nzima akimtakia Ferguson kurejea katika hali yake ya kawaida ya uimara haraka iwezekanavyo.

Post a Comment