Dkt. Mwigulu Nchemba ataka matumizi ya teknolojia kudhibiti uhalifu wa Kimataifa


Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni hitaji la lazima katika kukabiliana na uhalifu wa kimataifa unaopangwa ambao kwa sasa unatumia mbinu tata za kidijitali kuvuka mipaka ya mataifa. 

Akifungua Mkutano Mkuu wa 11 na Kongamano la Chama cha Waendesha Mashtaka Afrika Mashariki (EAAP) jijini Dar es Salaam  Mei 4, 2026, Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa aina nyingi za uhalifu wa kisasa hupangwa, hufadhiliwa, na kuratibiwa kwa njia za kielektroniki, jambo linalohitaji mifumo imara ya kiteknolojia na mshikamano wa vyombo vya dola ili kuudhibiti kwa ufanisi.

Waziri Mkuu ameeleza kuwa uhalifu dhidi ya wanyamapori na uhalifu mwingine uliopangwa ni tishio kubwa kwa uchumi, rasilimali, na usalama wa nchi, kwani wahalifu hutumia teknolojia kuficha mbinu zao na kuratibu athari zinazovuka mipaka kwa kasi kubwa. 

Alisisitiza kuwa vyombo vya haki jinai haviwezi kufanikiwa bila kuwa na mifumo madhubuti ya ushirikiano katika maeneo ya msaada wa kisheria na urejeshaji wa watuhumiwa, huku akitaja teknolojia kama nyenzo kuu ya kukabiliana na changamoto hiyo ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na duniani kote.

Katika hatua ya kuimarisha mapambano hayo, Dkt. Mwigulu amebainisha kuwa Serikali ya Tanzania imekuwa ikiboresha sheria zake ili kuruhusu matumizi ya ushahidi wa kidijitali, ufuatiliaji wa mawasiliano, na mbinu za kisasa za uchunguzi, sambamba na kuondoa urasimu katika utekelezaji wa maombi ya msaada wa kisheria. 

Alizitaka nchi wanachama wa EAAP kutumia jukwaa hilo kubadilishana taarifa na uzoefu ili kuhakikisha majibu ya nchi hizo dhidi ya uhalifu yanakuwa ya pamoja na ya kimkakati.

Mkutano huo wa siku tatu, wenye kaulimbiu inayolenga matumizi ya teknolojia dhidi ya uhalifu wa wanyamapori na uhalifu uliopangwa, unawakutanisha Wakurugenzi wa Mashtaka na viongozi wa sheria kutoka nchi wanachama 14, zikiwemo Tanzania, Kenya, Rwanda, na Uganda. 

No comments