SIFA NA UZOEFU VYAMBEBA DK. MUNISI UTEUZI WA NAIBU WAZIRI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amebainisha kuwa uteuzi wa Dkt. Evaline Wilbard Munisi kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano umechagizwa na sifa, uwezo, pamoja na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya umma na mahusiano.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumuapisha kiongozi huyo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo, Rais Samia ameeleza kuwa licha ya Dkt. Munisi kuwa Katibu Mkuu wa chama cha upinzani cha NCCR-Mageuzi, wasifu wake ulionyesha kuwa ana vigezo stahiki vya kuingia ndani ya Serikali ili kutoa mchango wake katika kulitumikia taifa.
Rais amesisitiza kuwa Watanzania wote wana wajibu wa kuunganisha nguvu zao katika kulitumikia taifa bila kujali tofauti zao za itikadi za vyama.
Rais Samia amemtaka Dkt. Munisi kushirikiana kwa karibu na viongozi pamoja na watendaji wa ofisi hiyo kusimamia upatikanaji wa kazi zenye staha na kulinda haki za wafanyakazi katika sekta za umma na binafsi.
Aidha, amemwelekeza kuweka mkazo katika kutafuta na kulinda fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania nje ya nchi, huku akihimiza kuimarishwa kwa mahusiano baina ya Serikali, waajiri, na waajiriwa. Ofisi hiyo pia imepewa jukumu la kukuza mahusiano ya kuheshimiana kati ya Serikali na mihimili mbalimbali ya dola kwa ajili ya ustawi wa nchi.
Rais Samia amewakumbusha viongozi wote walioapa kuwa vyeo walivyopewa ni dhamana ambazo Mungu amewawekea ili wawatumikie wananchi kwa nidhamu na unyenyekevu. Amewataka kuelekeza nguvu zao katika kutatua changamoto za wananchi na kuhakikisha utendaji wao unaleta matokeo yanayopimika. Rais amesisitiza kuwa dhamana ya uongozi inapaswa kutumika kama chombo cha huduma kwa jamii na si vinginevyo.
Kwa upande wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Rais Samia amemuapisha Mtendaji Mkuu, Dkt. Kheri Mahimbali, na kumtaka kuisimamia taasisi hiyo kwa weledi ili kurejesha ufanisi na imani ya wananchi.
Rais amebainisha kuwa uongozi wa TEMESA unapaswa kufanyia kazi changamoto na hoja zilizoibuliwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuleta matokeo chanya.
Viongozi wengine walioapa kiapo cha uadilifu ni pamoja na Balozi Ali Jabir Mwadini (Katibu wa Rais), Mhandisi Peter Philip Mwasalyanda (Mkurugenzi Mkuu TCRA), Dkt. Jabir Kuwe Bakari (Mkurugenzi Mkuu TCAA), na Mhe. Angela Charles Kizigha ambaye ni Mshauri wa Rais katika Masuala ya Jamii.
Post a Comment