MSONDO NGOMA YATAJA SIRI YA KUTUMBUIZA WIKI NZIMA BILA KUCHOKA


Bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma maarufu kama ‘Baba wa Muziki’, imeendelea kudhihirisha ukongwe wake kwa kuimarika zaidi kimuziki na kiutumbuizaji, huku ikisalia kuwa bendi pekee ya wazawa inayomudu kutumbuiza wiki nzima bila kuchoka. 

Meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti, amebainisha kuwa siri ya mafanikio hayo inatokana na bendi hiyo kujiendesha kama taasisi kamili ambapo kila hatua inapangwa kwa utafiti wa kina na makubaliano ya pamoja. 

Mfumo huo wa kitaasisi umewezesha bendi kuwa na ratiba iliyosheheni maonesho mengi hadi Julai mwaka huu, huku ikijikita katika kutoa muziki bora unaokidhi mahitaji ya mashabiki wa rika zote na kuhimili ushindani mkali sokoni.

Kwa upande wake, mdau wa muziki nchini, Jimmy Chika, ameeleza kuwa Msondo Ngoma imefanikiwa kurejesha heshima ya muziki wa dansi kwa kuchanganya vijana wenye damu changa na wanamuziki wakongwe. 

Ushirikiano huo umezalisha ladha ya kipekee inayovutia mazingira ya sasa ya soko la muziki nchini. Katika kuendeleza kasi hiyo, bendi hiyo mwaka huu imerekodi nyimbo mbili mpya ambazo ni ‘Jirekebishe’ na ‘Hujafa Hujaumbika’. 

Kazi hizo mpya zimebeba ufundi wa kizazi kipya huku zikichagizwa na uzoefu wa wakongwe waliobaki imara kama Roman Mngande ‘Romario’, Ally Rajabu ‘Kiefu’, Abdul Pangamawe ‘Totoo’, na Mustafa Hamisi ‘Mustafa Pishuu’.

Pamoja na kuja na kazi hizo mpya, bendi hiyo inaendelea kufurahia mafanikio ya kazi zake za zamani ambazo bado zina heshima kubwa miongoni mwa mashabiki. Nyimbo kama ‘Mwanamkiwa’, ‘Kilio cha Mtu Mzima’, na ‘Kaza Moyo’ zimeendelea kung’ara na kupendwa zaidi, hali inayothibitisha kuwa bendi hiyo imefanikiwa kutengeneza kazi zisizochuja. 

Kwa kuzingatia ratiba yao na ubora wa kazi zao, Msondo Ngoma inaendelea kubaki kuwa moja ya nguzo muhimu katika uhai wa muziki wa dansi nchini Tanzania.

No comments