SERIKALI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA TAASISI ZA DINI KUIMARISHA AMANI NA MAADILI NCHINI
︎ Asema dini ni nguzo muhimu ya malezi na mshikamano wa Taifa
︎ Asisitiza jamii kuendelea kuombea na kulinda amani ya nchiWaziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi za dini nchini ili kuimarisha maadili, mshikamano wa kijamii na kudumisha amani ambayo ni msingi wa maendeleo endelevu ya Taifa.
Amesema hayo leo Jumapili, Mei 3, 2026, aliposhiriki ibada katika Kanisa Kuu la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mufindi, lililopo Mafinga Mjini, mkoani Iringa.
Akizungumza na waumini, Dkt. Nchemba amesema taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye maadili mema, inayozingatia misingi ya haki na uwajibikaji.
“Serikali inaendelea kusisitiza Watanzania wote kuwa wadau wa kuombea na kusimamia amani ya nchi yetu,” amesema.
Ameongeza kuwa mafanikio ya mipango ya maendeleo ya Taifa yanategemea uwepo wa amani.
“Pasipokuwa na amani, hata malengo binafsi ya mtu mmoja mmoja ya Mtanzania mmoja mmoja hayawezi kufikiwa,” amesema.
Waziri Mkuu pia ameeleza mabadiliko ya mazingira ya dunia na changamoto zinazoweza kujitokeza.
“Kuna aina mpya ya mapambano, na mapambano hayo ni ya rasilimali na kila palipo na rasilimali mara nyingi huwa kunavutia maadui na hupenda kupitia migawanyiko ya raia wa nchi hizo husika,” amesema.
Katika hatua nyingine, amepongeza juhudi za Kanisa katika malezi ya watoto na vijana.
“Maandalizi ya watoto hivi si tu manufaa kwa Kanisa, ni manufaa pia kwa Taifa tunalolitaka,” amesema.
Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mufindi, Dkt. Anthony Kipangula, ameipongeza Serikali kwa kazi ya kuwahudumia wananchi na kusisitiza kuwa ziara za Waziri Mkuu zimeonesha uongozi unaowagusa wananchi moja kwa moja.
“Nimeona juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuwajali wananchi mtu wa ngazi yako kushuka mpaka kusikiliza kesi ya mwananchi na kumruhusu ajieleze, niliona ni maajabu kabisa,” amesema.
Ameongeza kuwa Kanisa litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha maadili mema, kutoa ushauri na kuliombea Taifa ili kudumisha amani na ustawi wa jamii.

Post a Comment