HOJA NZITO: KWA NINI RIPOTI YA JAJI CHANDE HAIJAWATAJA KWA MAJINA WALIOHUSIKA NA UPIGAJI RISASI?




Ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Siku na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, imeendelea kuibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi, hasa kuhusu suala la uwajibikaji kwa waliohusika kuwapiga watu risasi.

Licha ya Tume hiyo kuthibitisha kuwepo kwa vifo vilivyotokana na matumizi ya risasi, kumeibuka maswali mengi juu ya sababu za ripoti hiyo kutowataja waziwazi waliohusika na kwa nini hatua za haraka za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao. 

Katikati ya maswali hayo, kumeonekana kuwepo kwa wimbi la upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii, unaochochewa na baadhi ya watu waliotarajia ripoti hiyo kuelekeza lawama na uwajibikaji wa moja kwa moja kwa vyombo vilivyodhibiti vurugu, ambazo zilisababisha hasara ya kiuchumi inayokadiriwa kufika shilingi bilioni 125 kutokana na uharibifu wa mali za serikali na raia.

Akifafanua utata huo wakati wa mkutano na wahariri jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Jaji Mohamed Chande Othman ameweka wazi kuwa hadidu za rejea za Tume yake zilikuwa ni kuchunguza vyanzo vya ghasia, mazingira ya matukio, na kutoa mapendekezo, na si kutoa hukumu ya kijinai. Amesema, "Kwa mujibu wa hadidu za rejea za Tume ya Uchunguzi, jukumu la Tume lilikuwa ni kuchunguza na kubainisha chanzo halisi cha ghasia, malengo ya waliohusika, mazingira ya matukio, hatua zilizochukuliwa na kutoa mapendekezo. Tume sio chombo cha kutoa hatia ya jinai dhidi ya mtu binafsi; utambuzi wa wahusika na kuwawajibisha katika jinai kunahitaji uchunguzi wa kijinai katika viwango vya ushahidi unaotakiwa kuthibitishwa mahakamani." Jaji Chande alisisitiza kuwa uwajibikaji wa kijinai unahitaji uthibitisho wa pasi na shaka, jambo ambalo linapaswa kufanywa na vyombo maalum vya upelelezi.

Kutokana na misingi hiyo ya kisheria, Tume ya Jaji Chande imependekeza kuundwa kwa chombo maalum kitakachofanya upelelezi wa kina kwa wale wote wanaotuhumiwa ili wakibainika wafikishwe mbele ya sheria. 

Jaji Chande amebainisha kuwa uwajibikaji huo unapaswa kuwagusa wote waliohusika, kuanzia waliopanga, walioratibu, waliofadhili, na waliochochea ghasia hizo, na si tu wale waliokuwa mstari wa mbele kudhibiti vurugu. 

Msimamo huu unatajwa kuwagusa wale wanaotumia mitandao ya kijamii kupotosha ukweli kwa lengo la kulinda maslahi yao, ambapo Jaji Mkuu Mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, amewapa changamoto wakosoaji wa ripoti hiyo akisema, "Kama mnaipinga ripoti, leteni hoja zenu kwa uchunguzi mlioufanya nyie kisayansi na mueleze mbinu mliyotumia kupata matokeo yenu yanayopinga matokeo ya Tume."

No comments