Serengeti Boys Watakata Morocco: Watinga Nusu Fainali AFCON
Timu ya Taifa ya wavulana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, imeandika ukurasa mpya na wa kihistoria katika soka la Tanzania baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) nchini Morocco kwa kuitoboa Algeria kwa penalti 4-3.
Katika mtanange wa kusisimua uliopigwa kwenye Uwanja wa Mohammed VI, vijana hao walionesha ukomavu mkubwa na utulivu wa hali ya juu wa kimchezo kwa kumaliza dakika 90 za kawaida kwa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Algeria na hivyo kuenda katika matuta.
Ushindi huo umewavusha Serengeti hadi nne bora barani Afrik ,na pia umewakatia rasmi tiketi ya kuelekea nchini Qatar kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 13 mwaka huu.
Mafanikio haya ya Serengeti Boys yanabaki kuwa historia ya kipekee na ya kiwango cha juu miongoni mwa timu za taifa msimu huu, wakivunja mwiko wa timu za nyuma zilizoshindwa kufika hatua ya nusu fainali.
Kumbukumbu zinaonesha kuwa wakubwa zao, Taifa Stars, waliishia hatua ya 16 bora katika fainali za AFCON zilizofanyika Morocco mwaka 2025, huku dada zao, Serengeti Girls, wakiishia robo fainali ya Kombe la Dunia kule India mwaka 2022.
Baada ya miaka kadhaa ya kujitafuta, ikiwemo kushiriki michuano ya AFCON mara tatu zilizopita mwaka 2017, 2019 na 2025 bila kufanikiwa kuvuka hatua ya makundi, safari hii vijana wameonesha dhamira ya dhati ya kubadili upepo wa soka la vijana nchini na kupeperusha vyema bendera ya nchi.
Safari ya Serengeti Boys kuelekea hatua hii ngumu ya robo fainali ilijengwa na matokeo mchanganyiko katika hatua ya makundi, ambapo walizisambaratisha timu za Msumbiji na Angola kwa jumla ya mabao 3-0 kila mmoja, kabla ya kukumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Mali.
Post a Comment