Kwa Nini Klabu Zinapaswa Kusajili kwa Malengo ?
Mchakato wa usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa 2026/2027 unaendelea kushika kasi katika klabu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League, Ligi Kuu ya Vijana chini ya umri wa miaka 20, na Ligi Kuu ya Wanawake, huku madirisha yakifungwa Agosti 15 saa 5:59 usiku bila nyongeza yoyote.
Katika kipindi hiki cha ushindani mkubwa ambapo klabu zinapigana vikumbo kuwania saini za wachezaji, ni muhimu sana kwa viongozi wa vilabu kuachana na usajili wa mazoea au wa mihemko ya kisiasa, na badala yake zikusudie kusajili kwa malengo madhubuti.
Usajili wenye malengo ndio msingi mkuu utakaowezesha klabu kupata matokeo bora si tu kwenye ligi ya ndani, bali pia katika mashindano ya kimataifa, kwani kila pesa inayowekkezwa inapaswa kuleta tija inayolingana na malengo ya kiushindani ya timu husika.
Pamoja na usajili wa malengo, klabu zinapaswa kutambua kuwa kujidanganya au kuruka taratibu wakati wa kuwasilisha nyaraka kupitia mfumo wa FIFA Connect kunaweza kuingiza timu kwenye migogoro mikubwa isiyo ya lazima na wachezaji au klabu zingine.
Ni wajibu wa kila klabu kuhakikisha inafuata kanuni, sheria, na taratibu zote zilizowekwa katika uwasilishaji wa nyaraka kama vile mikataba ya ajira, hati za kusafiria, vyeti vya afya, na vibali vya kazi kwa wachezaji wa nje, ili kuepuka ucheleweshaji na adhabu za kikanuni. Uzingatiaji thabiti wa sheria hizi unaleta utulivu wa kimitendaji na kujenga taswira nzuri ya kistaarabu katika uendeshaji wa soka letu la kisasa.
Eneo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee na klabu zote ni utekelezaji mkali wa Kanuni ya 62(4) ya Ligi Kuu Tanzania, inayoeleza wazi kuwa wachezaji wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa ni wale tu wanaocheza katika timu za taifa za nchi zao.
Uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kupitia kwa Rais wake Wallace Karia, umesisitiza kuwa watatilia mkazo mkubwa kanuni hii kutokana na changamoto zilizokuwepo hapo nyuma, ambapo klabu zilikuwa zikitumia mianya kusajili wachezaji wa kigeni ambao hawana sifa ya kucheza timu za taifa za nchi zao kwa kisingizio tu cha kutoka ligi za nchi nyingine.
Hatua hii inalenga kulinda ubora wa ushindani na kuendana na maono ya kitaifa yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Januari 10, 2026, alipoeleza wazi kuwa ni wajibu wa wote kuhakikisha maandalizi ya AFCON 2027 yanafanyika kwa ufanisi mkubwa kwa kuwekeza katika vipaji vitakavyoimarisha soka letu na kuwapa wachezaji uzoefu wa kutosha.

Post a Comment