Umoja wa Kitaifa: Wazee na JMAT Shinyanga Washirikiana Kulinda Amani ya Nchi kwa Kuunda Kamati 17
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Manispaa ya Shinyanga, Stephano Tano amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kushikamana katika kulinda umoja wa taifa kama alivyoelekeza Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere kuwa ulinzi wa nchi ni jukumu la kila mtanzania mzalendo.
Kauli hiyo imekuja wakati akizungumzia mkakati mpya wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Mkoani Shinyanga, ambayo katika kuimarisha harakati za kuhubiri amani na mshikamano wa kijamii, imeanzisha kamati ndogo ndogo 17 zitakazosaidia kusimamia, kuratibu na kuongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo ndani ya mkoa huo.
Mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Balilusa Khamis, amefafanua kuwa hatua ya kuunda kamati hizo inalenga kuhakikisha jumuiya inawafikia wananchi wengi zaidi kupitia elimu ya amani, maridhiano na upendo, ambapo zitakuwa na jukumu la kuhamasisha maadili mema na kujenga mazingira ya utulivu miongoni mwa jamii.
Sheikh Balilusa amesisitiza kuwa suala la maridhiano ni muhimu katika maisha ya kila siku na kwamba jumuiya hiyo haibagui dini, kabila wala mila kwani imewakutanisha pamoja viongozi wa dini zote na viongozi wa kimila kwa lengo la kujenga umoja wa kitaifa na kushirikiana na wadau wote bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa au kijamii.
Naye mjumbe wa kamati ya JMAT, Anna Mwalongo ameunga mkono mwelekeo huo akieleza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa maisha bora na maendeleo ya jamii, kwani mali, familia na mafanikio yote ya mwanadamu yanapoteza maana ikiwa hakuna utulivu nchini. Kutokana na muktadha huo, Mwalongo ametoa wito kwa wananchi mkoani humo na Tanzania kwa ujumla kuendelea kulinda kwa wivu mkubwa tunu za taifa kwa kudumisha upendo, mshikamano na maridhiano ili kuiwezesha nchi kusonga mbele ikiwa na umoja thabiti.
Post a Comment