Benki ya CRDB kuandaa kituo maalumu cha kuendeleza vipaji vya Ndondo Cup
Benki ya CRDB imetangaza mpango wa kuanzisha kituo maalumu kitakacholenga kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wachezaji wa soka wanaong'ara katika mashindano ya Imbeju Ndondo Cup ili kuwapa fursa ya kufikia soka la ushindani ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa, baada ya mchezo wa ufunguzi wa msimu wa 13 wa mashindano hayo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, ambapo timu ya Madenge iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mzimuni.
Tully alieleza kuwa uwekezaji wa Sh milioni 400 uliofanywa na benki hiyo unalenga kuwapa nafasi vijana wenye vipaji wanaokosa fursa ya kuonekana na kueleza kuwa atazungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Abdulmajid Nsekela, kuhusu kuanzishwa kwa Imbeju Football Academy au CRDB Foundation Academy ili kukuza vipaji hivyo na kutumia michezo kama nyenzo ya kuwawezesha vijana kiuchumi na ajira.
“Nimefurahishwa na mwitikio mkubwa wa mashabiki waliofurika katika Uwanja wa KMC, lakini kikubwa zaidi ni kiwango cha wachezaji walichokionyesha katika mchezo wa ufunguzi,” alisema Tully
Katika mchezo huo, bao pekee la Madenge, iliyokuwa chini ya kocha Idd Moshi, lilifungwa na Fadhil Nado dakika ya 39, huku Ardason Chawaka akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi. Katika mchezo huo, timu ya Mzimuni, iliyokuwa ikinolewa na mchezaji wa zamani wa Yanga, Athumani Idd ‘Chuji’, ilishindwa kuhimili kasi ya wapinzani wake licha ya kumtumia kiungo mpya wa Yanga, Juma Issa Abushiri, aliyejiunga na timu hiyo akitokea Fountain Gate.

Post a Comment