Rais Samia Aondoka Nchini Kwenda Ghana
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameondoka nchini leo tarehe 21 Julai, 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Jijini Dar es Salaam kuelekea Accra, nchini Ghana, kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Katika ziara hiyo atashiriki Mkutano Mkuu Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu afya utakaofanyika tarehe 22 Julai, 2026 jijini humo.
Katika mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo "Kuendeleza Haki, Usawa na Huduma za Afya kwa Wote," viongozi watatafakari na kujadili hatua za pamoja za kutokomeza magonjwa ya UKIMWI na Kifua Kikuu, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuiliwa vya wajawazito na watoto, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika kwa ujumla.

Post a Comment