WAZIRI SANGU:UANAGENZI KUWATOA VIJANA KIMAISHA
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuimarisha programu ya mafunzo ya uanagenzi kama mkakati wa kuwajengea vijana stadi za kazi zitakazowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine, hatua inayolenga kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mheshimiwa Deus Sangu amesema hayo jana Julai 18, 2026 wakati alipokagua utekelezaji wa mafunzo ya uanagenzi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Kampasi ya Rukwa.
Waziri Sangu alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26 Serikali, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewezesha vijana 5,746 kupata mafunzo ya uanagenzi katika vyuo 46 nchini huku ikigharamia ada za mafunzo, bima ya afya na nauli za mafunzo kwa vitendo.
Alieleza kuwa uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Aidha, aliwahakikishia vijana kuwa Serikali itaendelea kutafuta fursa za ajira ndani na nje ya nchi ili kuongeza nafasi za ajira kwa wahitimu wa programu hiyo.
Waziri Sangu pia alitangaza kuwa kuanzia mwaka 2026 wahitimu wa mafunzo ya uanagenzi wataanza kupatiwa vifaa vya kuanzia kazi (start-up tools) ili kuwawezesha kujiajiri mara baada ya kuhitimu na kuongeza mchango wao katika uzalishaji na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mheshimiwa Nyakia Ally Chirukie ameipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuratibu mafunzo hayo ambayo yamekuwa chachu ya kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiri wenzao.
Naye, Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Alana Nchimbi alisema mkoa wa Rukwa una vyuo viwili vinavyotekeleza programu ya uanagenzi kwa mwaka 2025/26 ambavyo ni MUST Kampasi ya Rukwa yenye wanagenzi 154 na Chuo cha Kilimo na Mifugo Laela chenye wanagenzi 120.
Mkuu wa MUST Kampasi ya Rukwa, Prof. Asheri Mwidege alisema mafunzo hayo yamewawezesha wanagenzi kupata umahiri wa vitendo ambapo wamefanikiwa kutengeneza mageti na kushiriki ukarabati wa hosteli za wasichana ndani ya chuo.
Prof. Mwidege aliishukuru Serikali kwa kugharamia bima ya afya kwa wanagenzi wote 154 wa kampasi hiyo pamoja na kugharamia kwa asilimia 100 nauli za kwenda katika maeneo ya mafunzo kwa vitendo hatua aliyosema imeongeza ari na ushiriki wa vijana katika programu hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanagenzi, Digna Sebastian John mhitimu wa Shahada ya Kwanza ya Sanaa katika Utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2021 ambaye sasa anasomea ufundi bomba alisema mafunzo hayo yamempa ujuzi unaomwezesha kujiajiri na kwamba programu hiyo imekuwa suluhisho la changamoto ya ajira kwa vijana wengi.
Naye mwanagenzi Ismail William Mbogo alisema ndani ya miezi sita ya mafunzo darasani wamejenga uwezo wa kufanya kazi za ufundi na tayari baadhi yao wanapata ajira za muda katika vijiji vinavyozunguka chuo. Alieleza kuwa kabla ya kujiunga na programu hiyo alikuwa akijishughulisha na kilimo cha mpunga katika Bonde la Ziwa Rukwa.
“Kabla ya hapa nilikuwa mkulima wa zao la mpunga kule bonde la ziwa Rukwa. Ufundi huu nimekuja kuujua hapa chuoni MUST kupitia mafunzo ya uanagenzi” alieleza ushuhuda huo kijana Mbogo mbele ya Waziri Sangu.








Post a Comment