Mbio za Mbuzi za Rotary Oysterbay Kukusanya Sh Milioni 250


Rais wa Rotary club , Philippe Demoulin, akiwa pamoja na wanafunzi wanufaika wa scholarship ya Rotary Club of Osterbay



Mbio za mbuzi za mwaka 2026 zinazoandaliwa na Klabu ya Rotary Oysterbay ya Dar es Salaam zimepanga kukusanya kiasi cha Shilingi milioni 250 kwa ajili ya kupanua fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania wenye uhitaji mkubwa wanaoendelea na masomo ya juu. 

Mbio hizo za kila mwaka za hisani, ambazo kwa mara ya kwanza zilianza kufanyika mwaka 2018 na kukua na kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya kijamii na uchangishaji fedha, safari hii zimepangwa kufanyika Septemba 19, 2026 katika Viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam. 

Hatua hiyo ya kubadili eneo la tukio kutoka Oysterbay inatokana na kuingiliana kwa ratiba na shughuli za soka zilizopangwa kufanyika katika uwanja wa awali, ambapo uongozi umeeleza kuwa kuhamia Kijitonyama kunatoa fursa ya kutumia viwanja vikubwa zaidi ambavyo ni rahisi kufikiwa na kufahamika kwa wakazi wengi wa jiji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Rais wa Klabu ya Rotary ya Oysterbay, Philippe Demoulin, alifafanua kuwa mbio hizo ni jukwaa kuu la kukusanya rasilimali kwa ajili ya miradi ya kijamii, hasa ufadhili wa ada na mahitaji mengine ya kielimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya ufundi kutoka katika mazingira duni. 

Alibainisha kuwa mpango huo umeshuhudia ukuaji mkubwa katika miaka ya hivi karibuni ambapo idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka wanafunzi 26 mwaka 2023, hadi kufikia 43 mwaka 2024, na kisha kupanda hadi wanafunzi 92 mwaka 2025, huku jumla ya vijana waliokwisha kusaidiwa hadi sasa ikifikia 400. 

Demoulin aliongeza kuwa uteuzi wa wanafunzi hao unazingatia vigezo viwili vikuu ambavyo ni ufaulu mzuri wa kitaaluma pamoja na ukweli wa changamoto za kifedha zinazowakabili, lengo likiwa ni kuhakikisha vijana wenye vipaji hawaachi masomo kwa kukosa uwezo wa kiuchumi.

Katika toleo la mwaka jana, mbio hizo zilifanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi milioni 158 baada ya kukata gharama zote za maandalizi, fedha ambazo zilielekezwa moja kwa moja kwenye ada na mahitaji ya wanafunzi, na ndio maana kwa mwaka huu malengo yameongezwa kufikia Shilingi milioni 250 ili kuwafikia vijana wengi zaidi. 

Akishuhudia faida za udhamini huo, mmoja wa wanafunzi wanufaika, Emaculata Nkuba, alieleza jinsi alivyokuwa akihangaika kabla ya kupata msaada huo uliomuwezesha kuendelea na masomo yake kwa amani na utulivu baada ya kushindwa kulipia ada hapo awali. 

Nkuba alitoa wito na kushauri jamii, mashirika, na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kudhamini, kuchangia, na kushiriki katika mbio hizo za hisani ili kuwapa matumaini vijana wengine wengi wenye ndoto za kusoma lakini wanakwamikishwa na umaskini.

No comments