AFCON 2027: Hospitali ya Amana yaimarisha huduma za dharura kwa ushirikiano na Madaktari Wasio na Mipaka



Maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 yameifanya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Amana kuingia katika ushirikiano mkakati na shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ili kuboresha huduma za dharura. 

Taarifa ya ushirikiano huo imo katika jarida la Mtandaoni la hospitali hiyo la Dakika za Afya namba tatu la Julai 17,2026.

Katika Jarida hilo,Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Bryceson Kiwelu, alibainisha kuwa michezo hiyo itakayohusisha mikusanyiko mikubwa ya watu inahitaji utayari wa hali ya juu wa kitabibu, hivyo hospitali imejipanga kujinoa zaidi ili kuhakikisha inatoa huduma bora wakati wote wa michuano hiyo. 

Katika kuunga mkono jitihada hizo, Mkurugenzi Mkazi wa MSF, Bi. Dana Krause, alikutana na uongozi wa hospitali hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi bega kwa bega ili kuhakikisha huduma za dharura zinaendelea kuimarika. 

Ushirikiano huu unajenga msingi imara uliowekwa tangu mwaka jana, ambapo MSF ilileta wataalamu wakiwemo madaktari bingwa wa dharura, wauguzi, na madereva, hatua iliyoongeza nguvu kazi na ufanisi mkubwa katika kutoa huduma za afya kwa wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa haraka hospitalini hapo.

No comments