Kikwete Aitaka Afrika Kubadili Ahadi za Afya Kuwa Utekelezaji Wenye Bajeti
Na Mwandishi Maalumu , Accra, Ghana
Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Jakaya Mrisho Kikwete, amezitaka serikali za Afrika kuacha kutegemea matamko na ahadi zisizoambatana na utekelezaji, na badala yake kuweka fedha za ndani, uwajibikaji na matumizi ya ubunifu kuwa msingi wa ajenda ya afya ya bara hilo.
Wito huo ulimetolewa hivi karibuni mjini Accra, Ghana, wakati wa Mjadala wa Ngazi ya Juu wa Sera uliowakutanisha viongozi, mawaziri, watunga sera na wataalamu wa afya pembezoni mwa Mkutano Maalumu wa Umoja wa Afrika kuhusu Afya, uliolenga kuendeleza ajenda ya afya kupitia ufadhili wa ndani na uwajibikaji.
Dk Kikwete alieleza kuwa utegemezi wa muda mrefu wa misaada ya nje hauwezi tena kuendelea kuwa msingi mkuu wa mifumo ya afya ya Afrika, hasa kutokana na kupungua kwa misaada hiyo, kuongezeka kwa madeni ya serikali na mahitaji makubwa ya huduma bora.
“Ujumbe kutoka Eswatini hadi Accra ni mmoja: Afrika lazima izidi kugharamia, kuzalisha na kulinda mustakabali wake wa afya,” alisema huku akikumbusha miaka 25 tangu Azimio la Abuja la mwaka 2001.Azimio hilo lilizitaka nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kutenga angalau asilimia 15 ya bajeti zao za kitaifa kwa ajili ya afya.
Pamoja na kuwa katika miaka 25 ya Azimio hilo alibainisha kuwa nchi nyingi bado zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha huku bara hilo likibeba mzigo mzito wa magonjwa kama vile Ukimwi, kifua kikuu, malaria na magonjwa yasiyoambukiza, sambamba na viwango vya juu vya vifo vya wajawazito ambapo asilimia sabini ya vifo vyote duniani hutokea Afrika.
Alisema hali hiyo haiwezi kuelezwa kuwa ni kushindwa kwa sayansi, kwa sababu dunia tayari ina maarifa, dawa, vifaa na teknolojia zinazoweza kuzuia idadi kubwa ya vifo hivyo.
Kwa maoni yake, tatizo kubwa ni kushindwa kuyafikisha maarifa na teknolojia hizo kwa watu wanaozihitaji.
“Mama anaporudi nyumbani salama, ni kwa sababu fedha, ushahidi wa kisayansi na utoaji wa huduma vimefanikiwa kukutana,” alisema.
“Changamoto iliyo mbele ya mkutano huu si kuvumbua tena, bali ni kupeleka ubunifu uliopo kwa wananchi — kuutoa kwenye kumbi za mikutano na miradi ya majaribio na kuuweka mikononi mwa wauguzi, wakunga na wahudumu wa afya ya jamii wanaookoa maisha kila siku.”
Akizungumzia uzoefu wa Tanzania, Dk Kikwete alisema Wakfu wa Jakaya Mrisho Kikwete umeshirikiana na Wizara ya Afya pamoja na taasisi za kitaifa za utafiti kuchambua hali ya afya ya mama na mtoto na kuanzisha Mkutano wa Kitaifa wa Kisayansi unaofanyika kila baada ya miaka miwili.
Alisema katika kipindi hicho, vifo vya wajawazito nchini Tanzania vimepungua kutoka zaidi ya vifo 550 kwa kila watoto 100,000 wanaozaliwahai hadi vifo 104.
Dk Kikwete aliwasilisha katika mkutano huo vipaumbele vitano ambavyo ni : kuifanya afya kuwa uwekezajiwa kimkakati; kuongeza mapato ya ndani kupitia bima, kodi bunifu na matumizi yenye ufanisi; kulinda huduma muhimu wakati misaada
inapopungua; kuimarisha uwajibikaji; na kuongeza ushirikiano wa kikanda.
Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia Afya, Masuala ya Kibinadamu na Maendeleo ya Jamii, Balozi Amma Twum-Amoah, alisema mafanikio lazima yapimwe kwa mabadiliko yanayoonekana katika maisha ya wananchi.
“Vipaumbele vyetu lazima vionekane katika utekelezaji, na maendeleo yetu yapimwe kwa maboresho yanayopatikana katika maisha ya kila siku ya watu wetu,” alisema.
Katika mkutano huo, mfumo mpya wa African Renaissance Health Financing Insights Dashboard ulizinduliwa ili kusaidia serikali kufuatilia ahadi za kifedha, matumizi ya bajeti na kuimarisha uwajibikaji.
Dk Kikwete pia alionya dhidi ya utegemezi mkubwa wa dawa na chanjo zinazoagizwa kutoka nje, akihimiza nchi za Afrika kuunga mkono Wakala wa Dawa wa Afrika na kuwekeza katika uzalishaji wa ndani.
Aliitimisha kwa kuwasilisha vipaumbele vitano vya kimkakati na kuhimiza viongozi kuondoka na dhamira ya dhati ya kubadili ahadi kuwa bajeti, na bajeti kuwa matokeo yanayopimika yanayoboresha maisha ya wananchi.

Post a Comment