RAIS SAMIA AHIMIZA EAC KUJITEGEMEA ILI KUHESHIMIKA DUNIANI



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza umuhimu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujitegemea kiuchumi ili iweze kupata heshima inayostahili katika medani za kimataifa. 

Akizungumza wakati wa kufunga Jukwaa la Biashara kati ya Tanzania na Kenya katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Rais Samia alibainisha kuwa kizazi cha sasa kina jukumu kubwa la kuijenga jumuiya hiyo kuwa imara na inayojielewa. Aliongeza kuwa ni lazima mataifa wanachama yahakikishe EAC inasimama kulingana na matakwa ya watu wake na si kufuata masharti ya mataifa ya nje, huku akisisitiza kuwa muungano huo unapaswa kuwa kielelezo cha ukanda mkubwa wa kiuchumi.

Katika kutilia mkazo uhusiano wa kihistoria, Rais Samia alieleza kuwa Tanzania na Kenya zina muunganiko wa kipekee ambao hauwezi kugawanywa kirahisi, akionya kuwa choyo, ubinafsi, na kusikiliza maneno ya nje ndivyo vyanzo vikuu vya migawanyiko. 

Alifafanua kuwa changamoto za kiteknolojia na mitandao ya kijamii zisitumike kubomoa umoja huo, bali nchi hizo mbili lazima ziende pamoja kwa mwendo mmoja ili kuepuka mmoja kumpoteza mwingine njiani. 

Aidha, aliwataka viongozi na wananchi kudhibiti vitendo vya fujo vinavyofanywa na baadhi ya vijana kwa kisingizio cha jumuiya, akisisitiza kuwa demokrasia ya ukanda huu lazima iendane na mila pamoja na desturi za Kiafrika.

Rais Samia pia alitangaza azma ya Tanzania kurekebisha sheria mbalimbali za kibiashara zenye utata ili ziendane na mazingira ya sasa na kurahisisha uwekezaji baina ya nchi hizo mbili. 

Alihimiza kamati za biashara za pamoja kukutana mara kwa mara kutatua vikwazo vya kibiashara badala ya kusubiri ziara za viongozi wakuu wa nchi. Kwa upande wa wafanyabiashara, Rais aliwataka kulipa kodi kwa uaminifu ili serikali ipate uwezo wa kuboresha miundombinu, huku akiwaasa wale waliowekeza nchini Kenya kufuata sheria za nchi hiyo na kuongeza thamani ya bidhaa zao ili kutengeneza ajira kwa vijana.

No comments