TANZANIA YATAJA KIKOSI CHA WACHEZAJI 10 KUELEKEA CHESS OLYMPIAD UZBEKISTAN




Chama cha Mchezo wa Chess Tanzania (TACA) kimekitangaza rasmi kikosi cha wachezaji kumi watakaoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa ya 'Chess Olympiad' yaliyopangwa kufanyika nchini Uzbekistan, Septemba mwaka huu. 

Uteuzi huo umefuatia kumalizika kwa mchujo mkali wa siku tatu uliofanyika jijini Dar es Salaam, ulioshirikisha wachezaji wasomi na kuibua vipaji vipya vilivyoonesha uwezo mkubwa katika mchezo huo wa akili. 

Michuano hiyo ya Olympiad inatarajiwa kuwakutanisha wachezaji bora wa mchezo huo kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni, ambapo Tanzania itashiriki kwa lengo la kuonesha ushindani wa kiwango cha juu.

Katika upande wa wanaume, timu itawakilishwa na Parsa Nasser, Albert Njau, Sarota Patrick, Henry Marwa, pamoja na Rashid Sharif ambao walifanikiwa kuvuka mchujo huo. 

Kwa upande wa wanawake, wachezaji waliopata nafasi ya kupeperusha bendera ya Taifa ni Anahi Rishit Shah, Neema Adam, Bertha Mkude, Lissa Joseph, na Mariam Gwae. 

Ofisa Habari wa TACA, Mussa Mangula, ameeleza kuwa kiwango cha ushindani kilichooneshwa wakati wa mchakato huo ni kielelezo tosha cha kukua kwa mchezo wa Chess nchini na kwamba mchujo ulikuwa wa haki na uliozingatia sifa na uwezo wa kila mchezaji.

Baada ya kukamilika kwa uteuzi huo, TACA imethibitisha kuanza kwa maandalizi rasmi ambapo programu za mafunzo zinatarajiwa kuanza mara moja ili kuwanoa wachezaji hao kabla ya kuelekea nchini Uzbekistan. 

Chama hicho kimeeleza kuwa kinafanya kazi kwa ukaribu na wadau mbalimbali ili kuhakikisha timu inapatiwa mahitaji yote muhimu na maandalizi ya kutosha. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wachezaji hao wanakuwa na utayari wa kukabiliana na ushindani mkali wa kimataifa unaotarajiwa kwenye michuano hiyo mikubwa.

No comments