Amani na Utulivu Vyafungua Milango ya Utajiri: Bilioni 81 Kunufaisha Vijana 200 Kupitia BBT
Serikali imesisitiza kuwa juhudi zinazofanyika katika kulinda amani, maridhiano, na umoja wa kitaifa ni msingi mkuu wa kuwezesha miradi mikubwa ya maendeleo kutekelezeka kwa tija.
Katika kudhihirisha hilo, vijana 200 nchini wanatarajiwa kunufaika na fursa adhimu ya unenepeshaji wa mbuzi na kondoo kupitia mradi wa miaka mitano wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), unaotekelezwa katika Kituo cha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) wilayani Kongwa, mkoani Dodoma.
Akizungumza kwenye warsha ya utambulisho wa mradi huo hivi karibuni, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Fabian Madele, alisema mradi huo una thamani ya Shilingi Bilioni 81. Lengo kuu ni kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri katika mnyororo mzima wa thamani wa mifugo, ikiwemo uzalishaji wa malisho, uchakataji wa vyakula, na matumizi ya teknolojia ya kisasa, ili kuleta ustawi wa kiuchumi kwa kundi hilo na taifa kwa ujumla.
"Walengwa wakuu ni vijana ambao watapata ujuzi wa vitendo. Serikali inatarajia kuona vijana hawa wakigeuka kuwa sehemu ya suluhisho la ajira nchini kwa kuanzisha biashara zao za kisasa za mifugo mara baada ya mafunzo," alisema Dk. Madele.
Ili kuhakikisha vijana hao wanapiga hatua, serikali imeweka utaratibu wa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu pamoja na dhamana za mikopo baada ya kuhitimu mafunzo yao. Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini, Daudi Mayeji, aliongeza kuwa mradi huo una malengo mapana ya kufikia vijana 1,750 ndani ya miaka mitano, ambapo kijana mmoja atajengewa uwezo wa kuhudumia mbuzi 100 kwa wakati mmoja, huku ekari 2,000 zikiwa tayari zimetengwa kwa ajili ya malisho.
Kwa upande wake, uongozi wa Wilaya ya Kongwa kupitia kwa Ofisa Tarafa, Jeremiah Kabebwa, umeishukuru Wizara kwa kuleta mradi huo na kuahidi kusimamia vijana ili waichangamkie fursa hiyo kikamilifu. Mradi huu wa BBT ni kielelezo cha jinsi utulivu wa nchi unavyotoa nafasi kwa serikali kuwekeza mabilioni ya fedha kwenye miradi inayolenga kuwainua vijana kiuchumi.

Post a Comment