SAUTI YA MWANANCHI: AMANI NI UHURU WA KUFANYA KAZI BILA HOFU
Saidi Makele, mkazi wa Kivule jijini Dar es Salaam, ametoa ushuhuda mzito juu ya umuhimu wa kulinda amani ya nchi, akirejea nyakati ngumu zilizowahi kuitikisa Tanzania na kutishia ustawi wa wananchi.
Makele anakumbusha matukio ya huko nyuma, akitolea mfano hali iliyojitokeza mwezi Oktoba ambapo amani ilikaribia kutoweka na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa raia.
Anakumbuka namna amri za kutotoka nje baada ya saa 12 jioni zilivyoweka kizuizi kikubwa kwa watu wa kipato cha chini, hususani wafanyabiashara wa Kariakoo ambao kutokana na changamoto za usafiri, mara nyingi hufika maeneo yao kama Kivule saa nne au saa tano usiku, jambo ambalo liliwafanya wawe hatarini kukamatwa na polisi bila kuwa na makosa ya jinai.
Kwa mujibu wa Makele, amani ina maana pana zaidi ya kutokuwepo kwa vita; ni ule uhuru wa mtu kufanya shughuli zake za kila siku kama vile uendeshaji wa bodaboda, ukulima, au biashara ndogondogo bila kuwa na wasiwasi.
Anaelezea kuwa katika mazingira ya machafuko, hata watu wazima wenye umri mkubwa kama yeye hujikuta wakikimbia kwa uoga wanapoona askari, jambo ambalo ni hatari kwa afya na usalama wao kwani hawawezi kushindana na kasi ya vijana.
Makele anasisitiza kuwa pindi amani inapotoweka, hata kile kidogo alichonacho mwananchi kinapotea, akitolea mfano wa mama mwenye genge ambaye akisikia milio ya risasi hulazimika kukimbia na kuacha mali zake zikiibiwa na watu wasio na nia njema.
Kutokana na uzoefu huo wa kadhia, Makele ametoa rai kwa Serikali na jamii kwa ujumla kuendelea kutunza amani kwa kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia, marafiki, na jamaa.
Anasema kuwa amani ndiyo inayomruhusu mfanyabiashara sokoni kuuza samaki wake kwa utulivu na mwananchi kutembea kwa uhuru bila kuhofia kukamatwa na vyombo vya dola. Makele anasisitiza kuwa amani ni kitu kikubwa kinachopaswa kuthaminiwa na kila Mtanzania, kwani bila hiyo hakuna maendeleo, na badala yake ni unyonge na upotevu wa mali na utu wa mwanadamu.

Post a Comment