SHEKHE MAVUMBI: RIPOTI YA JAJI CHANDE NI CHACHU YA UMOJA, TUSONGE MBELE



Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ibrahim Mavumbi, ametoa wito kwa viongozi wa dini kote nchini kutumia majukwaa yao kuwajenga wananchi kisaikolojia na kuimarisha umoja wa kitaifa kufuatia kukamilika kwa ripoti ya Tume Maalum iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Akizungumzia ripoti hiyo iliyowasilishwa na mwenyekiti wa tume, Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman, Shekhe Mavumbi amepongeza weledi na umakini mkubwa uliotumika, akisisitiza kuwa yaliyomo yanatoa taswira chanya ya nchi na hayapaswi kuwatia hofu Watanzania.

Amesema kuwa wakati taifa likisubiri utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa, ni jukumu la viongozi wa kiroho kusisitiza kuwa yaliyopita yamepita na sasa ni wakati wa kulinda amani na mshikamano wa nchi.

Ripoti hiyo imekuja kutoa majibu ya kisayansi na kisheria baada ya mfululizo wa matukio yaliyogusa hisia za kitaifa na kimataifa, ikilenga kuleta uwazi na uwajibikaji ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama na wananchi wenyewe. 

Shekhe Mavumbi amebainisha kuwa kazi hiyo ya tume imegusa masuala mapana ya kitaifa na kikanda, hivyo inapaswa kutazamwa kama daraja la kuelekea kwenye maridhiano na si chanzo cha mfarakano. 

Amewahimiza Watanzania kuwa na subira wakati serikali ikichuja mapendekezo hayo kwa ajili ya utekelezaji, huku akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa maendeleo yoyote. 


No comments