RIPOTI YA JAJI CHANDE NI DARASA LA KIMATAIFA: KEJERI ZA MTANDAONI NI ZAO LA KUKOSA UELEWA
Tume hii haikuundwa kwa upendeleo bali ni matokeo ya utaratibu wa kitaalamu ambapo wajumbe wake walikula kiapo cha uaminifu na uhuru, jambo ambalo hata Mahakama Kuu ilishathibitisha uhalali wake kufuatia majaribio ya kisheria ya kuitikisa.
Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu Profesa Ibrahim Juma alisema hayo wakati tume ilipokutana na wahariri na waandishi wa Habari kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Aprili 28..
Aliwataka watu hao kurejea katika hoja za Mahakama Kuu kuhusu kesi iliyofunguliwa kupinga tume hiyo ambapo mahakama ilisema bayana kuwa tume hiyo ni halali na huru kufanya majukumu yake.
“Uamuzi wa mahakama ni mzuri kwa sababu umeonesha uhuru wa wajumbe wa tume kupitia viapo vyao.
Jaji Mkuu Mstaafu, Profesa Ibrahim Juma amesema ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa vurugu za Oktoba 29 iliyowasilishwa Aprili 23 imejengwa juu ya ushahidi wa kina uliokusanywa ndani ya siku 153 za kazi ya tume.
Ameeleza kuwa tume ilisikiliza mashahidi, ilichambua nyaraka mbalimbali na kufanya tafiti za kisheria ndani na nje ya nchi, hivyo haiwezi kufanana na mitazamo ya watu au makundi mengine.
Aidha, amesisitiza kuwa mapendekezo yaliyotolewa yanatokana na ushahidi wa moja kwa moja, si wa kubuni au kuangalia mambo kwa juu juu kinadharia.
Naye Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu, Mohamed Othman Chande akijibu swali la mwandishi aliyehoji kwanini tume inaendelea kutoa maelezo wakati imeshakabidhi taarifa yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, alisema tume hiyo sio kama mahakama kwamba baada ya hukumu haijadili tena kesi husika.
Alifafanua kuwa tume ina nafasi ya kuendelea kuelimisha umma kutokana na changamoto iliyolikuta taifa na kwamba baada ya uchunguzi wake tume ilibaini mambo mengi ambayo jamii inastahili kupewa taarifa kama sehemu ya kuziba ufa ili kuzuia hatari na kujenga upya taifa.
Ni bayana kuwa wanaoendeleza dhihaka mitandaoni wanafanya hivyo kwa upungufu wa elimu juu ya namna mifumo ya kisheria inavyofanya kazi, kwani tume imevuka mipaka ya hadidu za rejea kwa kufanya uchambuzi wa kisayansi ambao haujawahi kushuhudiwa huko nyuma.
Badala ya kuandika sentensi za kejeli kwenye majukwaa ya kijamii, wapinzani wa ripoti hii wanapaswa kusoma mbinu za kitaalamu (methodology) zilizotumika, ambazo zimeweka viwango vya juu vya uwazi na ukweli visivyoweza kufutwa na maneno ya vijiweni.

Post a Comment