Rais Samia amtumia salamu za pongezi Simbu kwa kutikisa Marekani



. Atwaa Nafasi ya Pili Boston Marathon 2026

, Avunja Rekodi ya Taifa kwa Kishindo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemtumia salamu za pongezi za dhati mwanariadha nyota, Sajinitaji Alphonce Felix Simbu, kwa kuandika historia mpya baada ya kushika nafasi ya pili na kuweka rekodi mpya ya Taifa katika Mashindano ya Kimataifa ya mbio za Boston (Boston Marathon) nchini Marekani. 

Akiandika katika Instagramu yake, Rais Samia ameeleza kuwa ushindi huo wa pili mfululizo kwa Simbu ni heshima kubwa kwa Taifa, huku akibainisha kuwa mwanariadha huyo ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania na kutangaza jina la nchi katika ulimwengu wa michezo, jambo ambalo ni chachu ya matumaini na hamasa kubwa kwa vijana wengi nchini.

Katika kilele hicho cha msisimko kilichofanyika Jumatatu, Aprili 20, 2026, Simbu alionyesha uwezo wa ajabu kwa kumaliza mbio hizo za kilomita 42 akitumia muda wa saa 2:02:47. Muda huo si tu umempa nafasi ya pili mfululizo, bali umeweka rekodi mpya ya kibinafsi na rekodi mpya ya kitaifa kwa upande wa Tanzania, ikiwa ni maboresho makubwa kutoka rekodi yake ya awali ya saa 2:04:38 aliyoiweka Valencia mwaka 2024. Mafanikio haya yanamfanya Simbu kuwa miongoni mwa wanariadha wachache duniani walioweza kumaliza mbio za Boston chini ya muda wa saa 2:03 katika historia ya miaka 130 ya mashindano hayo.

Mchuano huo ulikuwa wa vuta ni kuvute ambapo bingwa mtetezi, John Korir kutoka Kenya, aliibuka mshindi wa kwanza akitumia muda wa saa 2:01:52 na kuvunja rekodi ya dunia ya mashindano hayo. 

Hata hivyo, kishindo cha Simbu kiliwashangaza watazamaji baada ya kumshinda kwa kasi ya ajabu (sprint finish) Benson Kipruto wa Kenya katika hatua za mwisho, ambapo Kipruto alimaliza katika nafasi ya tatu kwa muda wa saa 2:02:50, akizidiwa sekunde tatu tu na Mtanzania huyo. 



Ushindi huo unathibitisha kuwa Simbu amekomaa kutaaluma na sasa ameingia katika daraja la wakimbiaji wasomi (Elite) wanaoweza kutawala mbio yoyote kubwa duniani.

Ufanisi huu wa Simbu unamfanya kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama Mtanzania wa tatu katika historia kufikia jukwaa la washindi (podium) kule Boston, akifuata nyayo za magwiji Juma Ikangaa (1989) na Gabriel Geay (2023). 

Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), wameipongeza hatua hiyo wakisema ni kielelezo cha juhudi, nidhamu na maandalizi bora, huku wakiamini kuwa ushindi huu utafungua milango zaidi kwa wanariadha chipukizi na kuvutia wadhamini wengi zaidi kuelekea mashindano ya dunia na michezo ya Olimpiki ijayo.

No comments