Mavunde:Miradi ya maendeleo ni kodi zenu muilinde idumu
Wananchi wametakiwa kuwa walinzi wa kwanza wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao kwa kutambua kuwa fedha zinazotumika kuitekeleza ni kodi zao, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha inalindwa na kudumu.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akikagua mradi wa maji wa Ushirika uliopo Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita, uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.05 na unaohudumia wakazi zaidi ya 21,000 katika vijiji sita vilivyopo Kata ya Ushirika.
Mavunde amesema mradi huo utachangia kuboresha huduma ya maji safi na salama, kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo salama pamoja na kuinua ustawi wa jamii.
Amesisitiza wananchi kutoa taarifa mara moja wanapoona mtu anayeharibu miundombinu ya mradi ili hatua stahiki zichukuliwe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.
Naye Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mbogwe, Mhandisi Rodrick Mbepera, amesema mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 2.05 ulianza kujengwa Aprili 2024 na kukamilika Aprili 2025.
Waziri Mavunde, ambaye pia ni mlezi wa shughuli za maendeleo mkoani Geita, anaendelea na ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo tayari ametembelea wilaya za Chato, Nyang’hwale na Mbogwe.

Post a Comment