Citibank Kuendelea Kushirikiana na Tanzania Kwenye Masoko ya Mitaji na Miundombinu

 



Benki ya Kimataifa ya Citibank imethibitisha nia yake ya dhati ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Tanzania, ikiwemo kutoa ushirikiano mkubwa katika masoko ya mitaji ya ndani na kimataifa, ufadhili wa miradi ya kimkakati ya miundombinu, na uwekezaji wa sekta binafsi.

Hayo yamejiri katika mkutano wa kimkakati uliofanyika jijini London, nchini Uingereza, kati ya Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, na Afisa Mkuu Mtendaji wa Citibank anayesimamia Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bwana Akin Dawodu.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kukuza zaidi uhusiano wa kifedha uliodumu tangu benki hiyo ianze shughuli zake nchini humo mwaka 1995.

Katika mazungumzo hayo yaliyowashirikisha pia Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Balozi Mbelwa Kairuki, na Kamishna wa Idara ya Deni la Serikali, Bw. Japhet Justne, viongozi hao walipitia uwezo wa nchi kukopesheka kimataifa na mipango ya kuanzisha hati fungani ya kimataifa ya Eurobond hapo mbeleni.

Aidha walizungumzia ufadhili wa mabenki ya mikopo ya usafirishaji, pamoja na mageuzi ya soko la mitaji.

Citibank ilikubali kuunga mkono Tanzania katika adhima yake ya kufikia masoko ya mitaji barani Ulaya, Marekani, Mashariki ya Kati na Asia, huku ikisifiwa kwa mchango wake katika ukuaji wa kiuchumi.

Waziri Balozi Omar aliwatangazia wawekezaji hao maendeleo makubwa ya kiuchumi nchini, akionesha ongezeko la uzalishaji wa umeme, ukarabati mkubwa wa bandari za Dar es Salaam, Tanga, na Mtwara, na upanuzi wa miundombinu ya anga, sambamba na kuanza kwa utekelezaji rasmi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuanzia Julai mwaka huu.





Alisema Dira hiyo imelenga kufikisha uchumi wa Tanzania kufikia dola za Marekani trilioni moja katika kipindi cha miaka 25 ijayo, ambapo asilimia 70 ya uwekezaji huo inatazamiwa kutoka sekta binafsi.

Vilevile, aligusia kukamilika kwa kiasi kikubwa kwa mazungumzo ya mradi mkubwa wa gesi asilia wa LNG wenye thamani ya dola bilioni 42 za Marekani.

Kuhusu mazingira ya biashara na kodi, Waziri huyo alieleza kuwa Serikali inafanyia kazi mapendekezo 284 yaliyotolewa na tume maalum zilizoundwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuboresha mfumo wa kodi na biashara, akisisitiza kuwa mageuzi yajayo yatajikita katika kupanua wigo wa kodi na kuimarisha rasilimali za ndani badala ya kuongeza mizigo kwa wananchi. Katika mkutano huo Balozi Omar alipendekeza kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali na Citibank utakaogusa masoko ya mitaji, ufadhili wa miundombinu, na uhamasishaji wa sekta binafsi ili kuharakisha maendeleo ya nchi.

No comments