TFF, JAB Kuimarisha Weledi wa Habari za Michezo
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kukuza weledi, maadili na taaluma ya uandishi wa habari za michezo kupitia mafunzo na programu za kuwajengea uwezo wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Akizungumza Julai 27, 2026, mara baada ya kuhitimisha kikao kazi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, kilichofanyika katika Ofisi za Bodi jijini Dar es Salaam, Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Bw. Clifford Mario Ndimbo, amesema kikao hicho kililenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili.
Ndimbo amesema JAB ndiyo mamlaka inayosimamia ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania Bara, huku TFF na Bodi ya Ligi zikiendelea kushirikiana kwa karibu na waandishi hao katika utekelezaji wa shughuli za mpira wa miguu.
“Tumekuwa na kikao kizuri kilichojadili namna bora ya kuendeleza ushirikiano kati ya TFF na JAB. Tumekubaliana kuandaa warsha na mafunzo mbalimbali yatakayowajengea uwezo Waandishi wa Habari za michezo pamoja na wachambuzi, kwa lengo la kuhakikisha taaluma inaendelea kuimarika na kuzingatia viwango vya weledi na maadili,” amesema Ndimbo.
Ameongeza kuwa TFF itaendelea kuandaa mafunzo kwa maafisa habari wa vilabu ili kuwaongezea uwezo wa kitaaluma, huku akiwahimiza wale ambao bado hawajapata ithibati kutoka JAB kukamilisha mchakato huo.
“Tutaendelea kuwa na warsha kwa maafisa habari wa vilabu. Tunawahimiza wale ambao bado hawajapata ithibati kuhakikisha wanaipata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya taaluma na maadili ya uandishi wa habari,” ameeleza Ndimbo.
Kwa upande wake, Wakili Kipangula amesema umuhimu wa kutoa mafunzo kwa makundi hayo umetokana na malalamiko kutoka kwa wadau kuhusu namna baadhi yao wanavyotekeleza majukumu yao pamoja na kuwapo kwa ukiukwaji wa maadili.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuimarisha ubora wa taarifa za michezo zinazowafikia wananchi, kuongeza weledi miongoni mwa Waandishi wa Habari, wachambuzi na maafisa habari wa vilabu, pamoja na kuchangia maendeleo ya sekta za habari na mpira wa miguu nchini.

Post a Comment