Rais Samia ataka uwekezaji wa ndani kwenye sekta ya afya Afrika
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwito kwa nchi za Afrika ziongeze uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya ili kujenga mifumo imara, endelevu na inayojitegemea katika usimamizi wa sekta hiyo.
Alisema hayo wakati alipohutubia Mkutano Maalumu wa Wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu afya uliofanyika jijini Accra, Ghana jana.
Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu imeeleza kuwa mkutano huo umejadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya afya ya Afrika kupitia usawa katika upatikanaji wa huduma, afya kwa wote, kutokomeza Ukimwi, kuboresha afya ya mama na mtoto na kukabili magonjwa yasiyoambukiza na yasiyopewa kipaumbele.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisema Tanzania imeanza kutekeleza Ramani ya Afya ya Umoja wa Afrika 2030 kwa kuiingiza katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2026/2027 – 2030/2031, ikijielekeza kwenye uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea katika huduma za afya. Aliongeza kuwa Afrika ina maarifa, rasilimaliwatu na uwezo wa kubadili mifumo yake ya afya, na kinachohitajika sasa ni utashi mkubwa wa kisiasa, uwekezaji wa ndani na mshikamano wa bara.
Akifafanua zaidi, Rais Samia alisema serikali imefanya mageuzi ya sera na sheria ili kuvutia uwekezaji na kurahisisha biashara, hatua zilizowezesha kuanzishwa kwa viwanda 13 vya uzalishaji dawa, huku wawekezaji 149 wakionesha nia ya kuwekeza nchini.
Alibainisha kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania imekuwa ya kwanza barani Afrika kufikia kiwango cha tatu cha ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa dawa wa Shirika la Afya Duniani, hatua inayotarajiwa kuharakisha uzalishaji wa dawa bora nchini na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Aidha, Rais Samia alisema serikali imeongeza bajeti ya sekta hiyo kutoka Sh trilioni 1.8 mwaka 2024/2025 hadi Sh trilioni 3.1 mwaka 2026/2027 sambamba na kuanzisha Bima ya Afya kwa Wote ili kuwawezesha wananchi, wakiwemo wenye kipato cha chini kupata huduma muhimu za afya kwa gharama nafuu.
Alieleza kuwa uwekezaji huo umewezesha kujengwa kwa hospitali 119 za wilaya, vituo 649 vya afya na zahanati zaidi ya 2,700 na kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya kutoka takribani 10,000 hadi 13,700 kufikia Machi mwaka huu.
Uboreshaji huo umechangia ongezeko la uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 65 hadi 86 na uzazi unaohudumiwa na wataalamu kutoka asilimia 66 hadi 85. Takwimu hizo zimeenda sambamba na kupungua kwa vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka 147 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000, wakati vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi vikipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000.
Akifungua mkutano huo, Rais wa Ghana, John Mahama alisema kupungua kwa ufadhili wa afya duniani kunapaswa kuwa fursa kwa Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani na kujenga mifumo ya afya inayojitegemea. Pamoja na hayo, Rais Mahama ameahidi kumuunga mkono Rais Samia katika utekelezaji wa jukumu lake la Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ili kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.


Post a Comment