RAIS SAMIA AFUNGUA UKURASA MPYA KWA MAMA LISHE, AMWAGA MAMILIONI YA MIKOPO



 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka mwelekeo mpya wa kurasimisha sekta ya Mama na Baba Lishe nchini, akiitaja kuwa ni mhimili muhimu wa uchumi wa wananchi unaozalisha ajira na kuimarisha ustawi wa familia nyingi mijini na vijijini.

Akizungumza wakati wa kufungua Kongamano la Kitaifa la Mama na Baba Lishe nchini katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Rais Samia amezielekeza Wizara, Mikoa na Halmashauri kote nchini kutenga maeneo rasmi ya biashara na kuboresha miundombinu ili kundi hilo lifanye kazi kwa hadhi na tija. 

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mafunzo ya lishe, usafi na matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za wapishi na walaji.




Katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais (Ikulu), Bakari Machumu, imeelezwa kuwa Rais amekabidhi hundi ya shilingi bilioni 94.1 (94,158,250,400) kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. 

Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi jumuishi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kongamano hilo ni hatua ya kihistoria ya kutambua mchango wa Mama na Baba Lishe, huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, akibainisha kuwa matumizi ya nishati safi yatawasaidia wajasiriamali hao kuondokana na magonjwa yatokanayo na moshi.







Nao wadau wa maendeleo kupitia kwa Mkurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, wameahidi kuendelea kutoa elimu ya usimamizi wa fedha na mitaji nafuu ili kukuza sekta hiyo. 

Katika tukio hilo, Umoja wa Mamalishe Tanzania (UMALITA) umemtunuku Rais Samia Tuzo ya Heshima kwa uongozi wake thabiti katika kampeni ya nishati safi ya kupikia barani Afrika na nchini.

No comments