Jamhuri yapangua hoja za Lissu kuhusu haki ya faragha Gerezani Ukonga



UPANDE wa Jamhuri umepinga hoja za Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, za kudai kunyimwa haki ya faragha katika Gereza la Ukonga mkoani Dar es Salaam.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Stanley Kalokola, alitoa pingamizi hilo mbele ya Jopo la Majaji watatu wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Dar es Salaam—wakihusisha Jaji Amir Mruma, Jaji Dk. Angelo Rumisha, na Jaji Dk. Evaristo Longopa—wakati akimuuliza maswali ya dodoso wakili wa utetezi, Paul Kisabo. Kalokola alidai kuwa Jeshi la Magereza lina mamlaka ya kisheria ya kukagua mawasiliano ya kinyaraka na kumkagua wakili, ndugu, au yeyote anayeingia katika eneo la magereza katika mazingira yanayolazimu kufanya hivyo.

Shauri hilo la kikatiba lilifunguliwa na mawakili wa utetezi Kulwa Maduhu, Paul Kisabo, na Nashon Mkungu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kamishna Mkuu wa Magereza, na Mkuu wa Gereza la Ukonga, likilenga kutaka ufumbuzi wa haki za kikatiba zinazodaiwa kukiukwa gerezani hapo. Akijibu malalamiko hayo, Wakili Kisabo alilalamikia utaratibu wa mawasiliano ya kifaragha kati ya mahabusu na mawakili wao kutofuatwa, na kuomba maofisa magereza kuacha tabia ya kusikiliza na kufuatilia mazungumzo yao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Ukonga, Andrew Shaban, alidai mbele ya jopo hilo kuwa hajawahi kupiga marufuku mawakili, viongozi wa CHADEMA, wala ndugu za Lissu kwenda kumtembelea, bali yeye anasimamia utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za magereza. Shaban alisisitiza kuwa yeye ndiye mwenye mamlaka ya kudhibiti shughuli za gereza hilo na ataendelea kutekeleza majukumu yake kwa jinsi atakavyoona inafaa ili kulinda usalama.

Naye Tundu Lissu alijitetea mahakamani hapo akidai kuwa kwa kuzingatia kifungu cha 29 cha Sheria ya Magereza kinachohusu kuwagawa wafungwa na mahabusu katika madaraja, yeye si mahabusu wa kukosa haki ya kutembelewa na kupewa msaada wa kisheria. Aliongeza kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 12 ya sheria hiyo, yeye hayupo kwenye kundi linalopaswa kusimamiwa kwa karibu kiasi cha askari kusikiliza mazungumzo yake na wageni, akisisitiza kuwa hakuna sheria inayokataza au kuweka utaratibu wa aina hiyo kwa wageni wake.

No comments