WADAU WAHAMASISHWA KUCHANGIA MADAWATI KWELA HUKU SANGU AKIGAWA ZAIDI YA 100
Wadau wa maendeleo ndani na nje ya mkoa wa Rukwa wamehamasishwa kuchangia upatikanaji wa madawati kwa ajili ya kuwezesha watoto kusoma kwenye mazingira wezeshi kwa ustawi wa taaluma.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na Mbunge wa Jimbo la Kwela ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu wakati akikabidhi madawati kwa shule za msingi katika jimbo hilo alipofanya ziara ya kikazi.
Katika ziara hiyo sangu alikabidhi madawati zaidi ya 100 kwa shule za msingi sita zenye thamani ya shilingi Milioni 60 ambayo ameyapata kupitia ufadhili ya Benki ya Taifa ya Biashara, NBC.
Waziri Sangu akizungumza kwenye moja ya mikutano yake na wananchi wa kijiji cha Nankanga tarafa ya Kipeta na kijiji cha Ilemba alisema ametoa msaada huo kuunga mkono jitihanda za wananchi katika kuchangia maendeleo ya elimu huku akisisitiza kuwa yeye ni mbunge wa vitendo anayependa vitu vinavyoonekana ili kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wabunge ya kutatua kero za wananchi.
Miongoni mwa shule zilizopokea madawati hayo ni pamoja na Kalumbaleza, Msia, Kimambo, Ilemba, Nankanga na Deusi Sangu sekondari.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani wa kata ya Mwadui Mahmood Leonce Mgweno alisema amepokea madawati toka Ofisi ya Mbunge na kwa tayari amefikisha shuleni na kumpongeza Mbunge Sangu kwa msaada.
Aidha wananchi wametumia fursa ya ziara ya mbunge Sangu kueleza kufurahishwa kwao na jitihada anazozifanya kuchangia maendeleo ya jimbo hilo ikiwemo msaada wa madawati.
Bwa.Thomas Nsandale ameishukuru Ofisi ya Mbunge kwa kuwezesha wa upatikanaji wa madawati ikiwa ni miongoni mwa vingi walivyopatiwa katika kipindi chote Mhe.Sangu akiwa Mbunge wa Jimbo la Kwela
“Sangu amefanya mambo mengi ambayo yanatufanya sisi wananchi kutokupunguza upendo juu yake na tunamuomba pia Madawati haya yasiwe ya mwisho kwa wananchi wake wa Kwela Bali iwe sababu ya muendelezo wa Maendeleo haya” amesema Nsandale.
Waziri Sangu alikuwa jimboni Kwela wilaya ya Sumbawanga kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.


Post a Comment