RAIS SAMIA AKUTANA NA UJUMBE WA MTANDAO WA VIONGOZI WANAWAKE AFRIKA




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 20 Aprili, 2026 amepokea ujumbe kutoka Mtandao wa Viongozi Wanawake Afrika (AFLN) katika Ikulu ya Dar es Salaam. 

Jambo la msingi ni kuwa ujumbe huo umeipongeza Tanzania kwa kurejesha hali ya amani na utulivu kufuatia matukio ya vurugu ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pamoja na juhudi za Serikali katika kulinda umoja wa kitaifa na kurejesha shughuli za kawaida za kiuchumi na kijamii. 

Viongozi hao wastaafu, akiwemo Rais Mstaafu wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf na Rais Mstaafu wa Ethiopia Sahle-Work Zewde, wamepongeza uongozi thabiti wa Rais Samia katika kuiongoza nchi katika kipindi kigumu bila kuyumbisha utendaji wa taasisi.

Katika mazungumzo hayo, ujumbe wa AFLN umesisitiza umuhimu wa kuendeleza mageuzi ya kisiasa na kiutawala ili kuimarisha demokrasia, uwajibikaji na ushirikishwaji wa wadau huku ukihimiza kukuza nafasi za uongozi kwa wanawake. 

Ujumbe huo pia umeeleza utayari wake wa kuisaidia Tanzania kulea kizazi kipya cha viongozi wanawake na kuweka mifumo itakayowawezesha kuzitumikia vizuri nafasi hizo.

 Kwa upande wake, Rais Samia ameushukuru ujumbe huo na kusisitiza dhamira ya Serikali ya kuendelea kulinda amani, kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, na kusukuma mbele mageuzi ya taasisi na utawala bora. 

Rais amehitimisha kwa kusema kuwa Tanzania itaendelea kupanua fursa za uongozi kwa wanawake na vijana huku ikishikilia misingi ya demokrasia, ushirikishwaji na maendeleo endelevu.

No comments