BMT KUTUNUKU MAUA KWA WANAMICHEZO BORA MEI 9
KASHIKASHI ya kusaka wababe wa michezo nchini kwa mwaka 2025 sasa imefika patamu baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kutangaza rasmi kuwa kilele cha ugawaji wa tuzo hizo kitafanyika Mei 9, 2026.
Shughuli hiyo ya kukata na shoka, ambayo ni msimu wa nne mfululizo, inatarajiwa kutikisa Jiji la Dar es Salaam katika ukumbi wa kisasa wa ‘The Super Dome’ Masaki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Prof. Mkumbukwa Mtambo, amesema safari hii tuzo zimeongezeka na kufikia makundi 21, huku kukiwa na nyongeza ya "Tuzo ya Mwanahabari Nguli wa Michezo" ili kutoa heshima kwa kalamu zilizotukuka.
"Lengo letu ni kuendelea kuwatambua na kuwaenzi mashujaa wetu waliopeperusha vyema bendera ya nchi kimataifa mwaka 2025. Tuzo hizi zimeongeza hamasa kubwa na kufanya michezo kuwa sehemu ya kukuza uchumi na mshikamano," alisema Prof. Mtambo.
Katika kile kinachoonekana kuongeza ladha ya msimu huu, wananchi wamepewa mamlaka ya kumchagua mchezaji wanayemkubali zaidi kupitia kipengele cha "People’s Choice Award".
Mashabiki watatakiwa kupiga kura kwa kutuma jina la mwanamichezo wanayempenda kupitia WhatsApp namba +255 689 525 363.
Kati ya vipengele 21 vinavyowaniwa ni pamoja na Mwanamichezo Bora wa kiume na kike, chipukizi, wanamichezo wenye ulemavu, makocha, waamuzi, na tuzo ya heshima kwa wanamichezo wa zamani (Legends).
Prof. Mtambo amehitimisha kwa kutoa rai kwa wadau na makampuni kujitokeza kuunga mkono tamasha hilo la aina yake.
Post a Comment